Home KITAIFA Rais Dk.Samia : Kituo kipya cha Biashara kuimarisha uchumi wa Nchi

Rais Dk.Samia : Kituo kipya cha Biashara kuimarisha uchumi wa Nchi

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki ( EACLC) ni hatua muhimu ya kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato ya serikali, ajira kwa vijana, na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akizungumza leo Agosti, 1 2025, wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, Rais .Dk Samia amesema mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya biashara na usafirishaji, hasa kwa kuchochea mauzo ya nje na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Amebainisha kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama kitovu cha biashara na usafirishaji kwa nchi zote za Afrika Mashariki kwa kuwaunganisha wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na walaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.

“Eneo hil lina maghala ya kisasa, ofisi za biashara, na huduma zote muhimu za usafirishaji zilizo katika sehemu moja, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama na muda wa kusafirisha mizigo,” amesema.

Ameeleza kuwa mradi huo unaendana na mkakati wa serikali wa kujenga uchumi wa kidijitali, kwani shughuli nyingi katika kituo hicho zitasimamiwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektroniki.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa kituo hicho katika kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kikanda na bara zima.

Amehimiza wadau wa sekta binafsi na wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha kituo hicho kinatumika ipasavyo kwa manufaa ya taifa kwani mafanikio ya mradi huu yatategemea mshirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi,hiyo ni fursa ya kipekee ya kuongeza thamani ya bidhaa, kukuza ajira, na kuongeza mapato ya taifa kupitia biashara ya ndani na nje.

Rais Dk .Samia amesema kuwa ujenzi wa Kituo chicho haukulenga kuleta ushindani kwa wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.

Amesema badala yake, kituo hicho kina dhamira ya kutoa elimu kuhusu uboreshaji wa mifumo ili kusaidia wafanyabiashara kupata faida zaidi na kuchangia mapato ya Serikali.

Pia amemuomba Mkurugenzi wa EACLC, Dkt. Lisa Wang Xiangyun, kuandaa mkutano kati ya wafanyabiashara wa Kariakoo na wa kituo hicho ili kutoa somo kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuendesha biashara, na hivyo kuepusha upotevu wa mapato ya Serikali.

“Kituo hichi kitachochea ushirikiano kati ya sekta binafsi za Tanzania na China, na kuhamasisha mauzo ya bidhaa zenye thamani zaidi kwenda masoko ya China na masoko mengine ya kimataifa,” amesema.

Naye Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, amesema kituo hicho kitawawezesha wafanyabiashara kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali kuboresha ufanisi na kurahisisha biashara zao,na kusisitiza kuwa bidhaa zote zitakazotoka kituoni hapo zitakuwa na viwango vinavyokubalika kimataifa, hatua itakayoongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kwenye soko la kimataifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Gilead Teri, amesema kituo hicho kitatoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 15,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 50,000, pamoja na kuchangia karibu Dola milioni 8.2 kwa mapato ya serikali kila mwaka.

Amesma Kituo hicho chenye maduka zaidi ya 2,000 na ofisi za kisasa kimejengwa wanatarajia ajira rasmi 15000 na zisizo rasmi 50000 ujenzi wa mradi huo umegharimu shilingi bilioni 282.7.

Ameongeza kuwa lengo la kituo hicho kurahisisha biashara, kuongeza mapato ya serikali, kuchochea upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza ushindani wa bandari ya Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC), Dkt. Lisa Wang Xiangyun, amesema kituo hicho kitapunguza gharama za uendeshaji wa biashara kikanda kwa asilimia 30 na kuongeza mapato ya serikali, sambamba na kutoa fursa ya kusafirisha mazao kama mahindi, maharage, kahawa, ufuta, korosho, asali na mvinyo kwenda masoko ya nje, ikiwemo China.

“Kituo hichi kikiingiza bidhaa mbalimbali kutoka China kama mitambo, hatua ambayo imetokana na uongozi thabiti wa Rais Dk. Samia katika mageuzi ya kiuchumi na kuvutia wawekezaji nchini,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Omary Said Shaban, amesisitiza kuwa mradi huo ni mpango wa utekelezaji wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kwa Afrika Mashariki, Kusini na Bara zima na kuhimiza wafanyabiashara kutumia kituo hicho kama chachu ya kuboresha biashara zao na sio kukiona kama mshindani, bali fursa ya kujifunza mbinu bora za kibiashara.

Awali akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewahakikishia wafanyabishara pamoja na wanunuzi watakaofanya shughuli zao katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo wilayani Ubungo kuwa Serikali imejipanga ipasavyo ili kuondoa changamoto za usafiri pamoja na umeme mkoani Dar es Salaam hasa katika kituo hicho.

Chalamila amesema kuna miradi mbalimbali ya upanuzi wa barabara pamoja na ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) huku akieleza kuwa hivi karibuni mabasi hayo yaendayo haraka yatawasili nchini na kuongezwa katika njia mbalimbali ambapo kati ya hayo mabasi 99 yatawasili mwezi huu wa Agosti na kupelekwa njia ya Mbagala na njia ya Kimara hadi Gerezani na mabasi 250 yatawasili mwezi Oktoba,2025.

Aidha, amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imejipanga kutatua changamoto za kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, na tayari miradi minne inatekelezwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme katika mkoa huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here