Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuzindua mfumo wa kusajili vyombo vya habari kuanzia 1 hadi 30 Septemba 2025 kwaajili ya kufanyia kazi zao wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Pia Tume imeahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa vyombo vya habari nchini katika kuhakikisha taarifa za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 zinapatikana kwa wakati na kwa usahihi.
Akizungumza Agosti, 4 2025 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima wakati akifungua mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika ukumbi wa Mlimani City .
“Mfumo huu utasaidia vyombo vya habari kupata vibali na vitambulisho rasmi vya waandishi wake kwa ajili ya kufanikisha kazi zao wakati wa Uchaguzi Mkuu,” ameeleza.

Amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi, Tume itashirikiana na waandishi wa habari kupitia njia mbalimbali ikiwemo kushiriki katika vipindi vya redio na televisheni, pamoja na kutoa taarifa rasmi kwa wakati unaofaa ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa habari za kweli na zisizo na upotoshaji.
“Tunaamini kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha habari zinazotolewa zinazingatia maadili ya uandishi wa habari na kuepuka maudhui yanayoweza kuchochea chuki au ghasia,” amesema Kailima.

Kufanyika kwa mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kumehitimisha mfululizo wa mikutano ya wadau ambayo ilianza tangu Julai 27 .2025, ambapo Tume ilikutana na viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, wawakilishi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na watayarishaji wa maudhui ya mtandaoni.