Home KITAIFA DC SHEKIMWERI:Wizara ya Katiba na Sheria kusaidia kupunguza migogoro Ardhi

DC SHEKIMWERI:Wizara ya Katiba na Sheria kusaidia kupunguza migogoro Ardhi

Na Mwandishi wetu,Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabiri Shekimweri, amesema kuwa ushiriki wa Wizara ya Katiba na Sheria katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea jijini Dodoma ni fursa muhimu ya kupunguza migogoro mbalimbali, hasa ya ardhi, ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa mkoa huo.

Akizungumza leo Agosti 6, 2025, mara baada ya kutembelea banda la wizara hiyo, Shekimweri alisema kuwa huduma zinazotolewa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia zina umuhimu mkubwa kwa jamii, ikizingatiwa kuwa bado kuna malalamiko mengi yanayohusiana na masuala ya ardhi.

Amesema Wizara hiyo si tu inasikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi, bali pia inawapa maarifa ya haki na wajibu wao kisheria, jambo litakalosaidia kuimarisha ustawi wa jamii na mshikamano.

“Nimefurahi sana kukuta banda la Wizara ya Katiba na Sheria linatoa huduma hii ya msaada wa kisheria lakini pia linatoa elimu. Natoa wito kwa wananchi wote wafike hapa kupata huduma na elimu ya utatuzi wa migogoro, hasa wanawake wajitokeze kwa wingi kujifunza masuala ya mirathi kwani mara nyingi wao ndio wahanga wakuu,” amesema Shekimweri.

Shekimweri amepongeza elimu ya Haki na Utawala Bora inayotolewa na wizara hiyo kwa wananchi, akisema ni jambo muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

“Tunaelekea katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu, hivyo elimu ya haki, wajibu na utawala bora ni muhimu kwa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu na kwa uelewa mpana katika mchakato huo wa kidemokrasia,” amesisitiza.

Wizara ya Katiba na Sheria ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nanenane kwa kutoa huduma za kisheria, elimu na ushauri kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kupeleka huduma karibu na wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here