📌Aridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo
📌Asema kukamilika kwake kutaimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme na kukidhi mahitaji ya ongezeko la umeme kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya pembezoni.
Na Agnes Njaala, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amefanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya miradi ya upanuzi wa vituo vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme vya Dege, Gongolamboto na Ubungo vilivyopo jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme kwa wakazi wa Dar es Salaam, Pwani na mikoa ya jirani kutokana na ongezeko la mahitaji ya umeme.

Katika kituo cha Dege, upanuzi unahusisha usimikaji wa transfoma mpya yenye uwezo wa 120MVA, kutoka 60MVA ya awali. Pia, mradi unajumuisha ujenzi wa njia za kusambaza umeme za kilovoti 33. Utekelezaji wake umefikia asilimia 56 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 2026.
Kituo cha Gongolamboto pia kinahusisha usimikaji wa transfoma mpya yenye uwezo wa 125MVA kutoka 50MVA ya awali ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 80 , wakati kituo cha Ubungo kinapanuliwa kwa usimikaji wa transfoma yenye uwezo mkubwa wa 300MVA.

Akizungumza leo Agosti 7 , 2025 baada ya ukaguzi huo Bw. Twange amebainisha kuwa miradi hiyo mitatu ni ya kimkakati kwa sababu inalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kutosha kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani.
“Hii ni sehemu ya kuhakikisha kuwa miundombinu ya TANESCO inaimarishwa ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadae, hasa katika mikoa yenye shughuli nyingi za kiuchumi kama Dar es Salaam,” amesema Twange.
Ameongeza kuwa Dar es Salaam ni mkoa mkubwa unaochangia kwa kiasi kikubwa katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na TANESCO, hivyo kuwa na huduma ya umeme wa uhakika ni msingi wa kuendesha shughuli za kiuchumi, kijamii na utoaji huduma muhimu kama elimu na afya.
Twange amewapongeza Wahandisi na Wasimamizi wa miradi hiyo kwa uwajibikaji na weledi, licha ya kufanya kazi katika mazingira yenye changamoto. Ameeleza kufurahishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, akisema inazingatia muda uliowekwa katika mikataba.

“Ninayo furaha kusema kuwa kazi zinaendelea vizuri. Nawahakikishia wakazi wa Dar es Salaam hususani wa Kigamboni kuwa, changamoto za umeme wanazokumbana nazo hivi sasa zitaisha mara tu miradi hii itakapokamilika,” amesisitiza.
Aidha, amefafanua kuwa upanuzi wa vituo vya Gongolamboto na Ubungo utawezesha usambazaji wa umeme wa uhakika pia kwa maeneo ya nje ya Dar es Salaam, yakiwemo mikoa ya Pwani na mingine ya jirani.
Twange amehitimisha kwa kusema kuwa ziara hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa TANESCO inakuwa tayari kuwahudumia wateja kwa ufanisi zaidi kwa kuimarisha miundombinu ya umeme kwa wakati.