Na Mwandishi wetu, Dodoma
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, leo Agosti ,10 2025 ameambatana na mgombea mwenza wake, Chausiku Khatibu Mohamed, kufika katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kuchukua fomu za uteuzi.

Fomu hizo za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha NLD zilikabidhiwa rasmi na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacob Mwambegele. Hafla hiyo ilifanyika kwa heshima na kwa kuzingatia utaratibu wa kisheria uliowekwa na Tume.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ramadhan Kailima, aliwakaribisha wagombea hao kwa niaba ya Tume na kueleza kuwa wamekidhi vigezo vya awali vinavyohitajika kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Doyo alisisitiza dhamira yake ya kupunguza matumizi makubwa ya serikali iwapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi. Alieleza kuwa moja ya hatua atakazochukua ni kupunguza matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi wa umma, akisema.
“Nimekuja kuchukua fomu ya uteuzi kwa kutumia bajaji leo, kama ishara ya kuwaunga mkono vijana wanaoishi maisha ya kawaida na wanaojitahidi kujikwamua kupitia kazi zao za ujasiriamali. Wastani wa maisha yao unapaswa kueleweka na kuungwa mkono na kila mmoja wetu, kuna haja ya kupunguza matumizi serikani ili tuwaunge mkono vijana wengi zaidi.”

Aidha, Doyo aliwasilisha vipaumbele vyake vinne ambavyo ametaja kuwa ni muarobaini wa changamoto za Watanzania, na ambavyo vitapewa kipaumbele katika serikani yake.
Kwa upande wake, Mgombea Mwenza wa Urais, Chausiku Khatibu Mohamed, aliendelea kuwashukuru wanachama wa NLD na Watanzania kwa ujumla kwa kuonesha imani, mshikamano na moyo wa kizalendo katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Tunaamini kuwa kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko chanya kwa taifa letu, huku tukiweka msingi wa amani na mshikamano wa kweli. Amani ndiyo nguzo na tunu ya taifa letu. Chama cha NLD kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu, bila kudhalilisha wala kutweza utu wa mtu yeyote,”amesema.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imepanga kufanya uteuzi rasmi wa wagombea wa nafasi ya Urais na Makamu wa Rais mnamo Agosti, 27 2025.