Home KITAIFA Serikali yafungua milango ya fursa kwa wakulima wa mwani

Serikali yafungua milango ya fursa kwa wakulima wa mwani

Na Mwandishi wetu, Tanga

SERIKALI imewataka wakulima wa mwani nchini kutumia mbinu bora na za kisasa za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuongeza ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hayo, yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Dk. James Kilabuko wakati akifunga mafunzo ya kujenga uwezo kwa vikundi vinavyojihusisha na kilimo cha mwani yaliyofanyika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kwa muda wa siku kumi na mbili kuanzia tarehe 04 hadi 15 Agosti,2025.

“Mafunzo mliyojifunza ya kilimo bora cha mwani yatawasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji na ubora wa mwani katika soko la ndani na nje ya nchi,” alisema na kuongeza kuwa, “Mafunzo ya uongezaji thamani, matumizi bora ya kemikali mnazotumia kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na mwani, vifungashio vya bidhaa, zitazoweza kuwatambulisha na kuzitangaza bidhaa zenu ndani na hata nje ya nchi, upatikanaji wa masoko ya mwan,” amesema Dk. Kilabuko.

Amesema lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa mwani ili kuongezea mnyororo wa thamani wa zao hilo nchini.

Vilevile, amewataka wakulima hao kujipangia utaratibu wa kufikisha maarifa waliyoyapata kwa wanakikundi wengine ambao hawakupata fursa ya kupata mafunzo hayo kwa kufanya mazoezi katika vikundi vyao hususani mafunzo ya wokozi na huduma ya kwanza majini.

“Mazingira ya kazi zenu ni katika maji, hivyo suala mlilojifunza la namna ya kujiokoa shambani ni muhimu sana, elimu hiyo itawasaidia katika kuokoa maisha yako binafsi pamoja na jirani yako pindi anapopata changamoto akiwa katika shughuli za kilimo shambani” Alisema na kuongeza kuwa,” “kile mlichojifunza muwafikishie na wenzenu ili kuwa na uwelewa wa pamoja katika kuboresha maslahi ya pamoja ya vikundi vyenu,”amesema.

Awali akitoa neno la utangulizi kuhusu mafunzo haya Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Kanali Selestine Masalamado amesema Kuwa mafunzo haya yaliyofanyika wilayani Mkinga ni awamu ya pili ya sehemu ya utekelezaji wa mwongozo wa kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika bahari na maziwa makuu kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo hayo uliozinduliwa Februari 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“sehemu ya kwanza ulitekelezwa katika Wilaya tatu ikiwa ni pamoja na Mafia, Pangani na Bagamoyo ambazo shughuli zake kuu za kiuchumi zinategemea mazao ya bahari kwa kutoa mafunzo kwa vikundi na vyama vya ushirika, ujenzi wa vichanja vya kukaushia dagaa, na ununuzi wa boti moja ya kisasa kwa ajili ya doria baharini,”amesema Kanali Masalamado.

Ameongezea kuwa Kutokana na Mafanikio Makubwa wa awamu ya kwanza wa mradi wa kuimarisha ulinzi na usalama , Serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wameendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha usalama majini kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa boti mbili za doria, ujenzi wa makaushio ya mwani na mashine ya kusaga mwani, pamoja na kutoa mafunzo elekezi kwa vikundi 26 vya wakulima wa mwani katika Wilaya ya Mkinga.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Rashid Karim Gembe amepongeza uwepo wa mafunzo na kutoa shukrani za dhati kwa wafadhili pamoja na waratibu wa mafunzo hayo yatakayo leta mapinduzi ya mnyororo wa thamani wa zao la mwani na kuwakomboa kiuchumi wakulima wa mwani, hivyo ameahidi kuendelea kuwashika mkono wakulima wa mwani kwa kuwahakikishia ushirikiano utakao wawezesha kuyafikia malengo kupitia zao hilo.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Maendelo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Saimon Nkonoki amesema kuwa, awamu ya pili ya sehemu ya mradi ambao umeanza kwa mafunzo wilayani Mkinga umepokelewa vizuri kwa muitikio na ushirikiano mkubwa ikiwa ni ishara ya utayari wa Serikali katika kuwahudumia wananchi wake.

“Tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa wadau mbali mbali wa maendeleo hapa nchini, huku tukitoa rai kwa vikundi vilivyonufaika na mafunzo haya kuyaishi kwa vitendo hasa yale ya vitendo tunaamini yatawasaidia sana,”amesema Nkonoki.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo haya wameshukuru mafunzo yaliyotolewa kwao huku wakieleza namna yatavyowasaidia wakulima wa zao la mwani kwa ujumla na kueleza yatawafaa wao na jamii nzima.

Akiongea kwa niaba ya washiriki wenzake Aisha Jumbe amesema, “tunaamini zao hili tunaenda kulipa heshima kwa kupitia mafunzo haya, ambapo tutakuwa na mbinu mpya za huduma za kifedha, kujua soko na mahitaji ya soko, uandaaji wa fedha na utunzaji wa fedha na hii itatusaidia katika hatua zote za kilimo hadi kufikia matokeo ya mwisho kwa watumiaji wa bidhaa zetu ikiwemo; sabuni za kuogea, kufua, kusafisha maliwato, dawa kwa magonjwa mbalimbali na nyingine nyingi;”.

Mafunzo hayo ya kuvijengea uwezo wa kilimo bora, usimamizi wa vikundi, usimamizi wa fedha,utunzaji kumbukumbu, kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao pamoja na masoko ya zao la mwani kwa vikundi vya wanawake na vijana vya wakulima wa zao la mwani wa Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga, yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa ufadhili wa Serikali ya Japan pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here