Na Mwandishi wetu
TANZANIA imewekwa katika nafasi ya kimkakati kunufaika na ushirikiano mpya kati ya Afrika na Singapore, hasa kutokana na rasilimali zake, soko kubwa la kikanda na nafasi yake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na SADC.

Katika Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Singapore (SAMEV) uliofanyika jijini Singapore, Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Dk. Vivian Balakrishnan, amesisitiza kuwa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika yatakuwa kitovu cha ushirikiano mpya katika nyanja za kidiplomasia, uchumi na maendeleo endelevu.
Akieleza maeneo ya kipaumbele, Dk. Balakrishnan ametaja sekta ambazo Tanzania itanufaika moja kwa moja zikiwemo masoko ya bidhaa za kilimo na madini, uwekezaji katika teknolojia na nishati jadidifu, pamoja na elimu na mafunzo kwa vijana.
Aidha, Tanzania inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya jitihada za pamoja za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kukuza uchumi wa kidijitali na buluu, sambamba na kuvutia uwekezaji katika viwanda na biashara.

Sababu zinazoweka Tanzania katika nafasi hiyo ni pamoja na nguvu kazi kubwa ya vijana walio wengi, ardhi yenye rutuba, rasilimali za madini, nafasi nzuri ya kijiografia, pamoja na uongozi wake katika ushirikiano wa kikanda kupitia AfCFTA, EAC na SADC.
Kwa mujibu wa Dkt. Balakrishnan, ushirikiano huu utakuwa nguzo ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za uchumi na biashara duniani, huku Singapore ikitazama Tanzania kama sehemu ya lango la uwekezaji barani Afrika.
Mkutano wa SAMEV hufanyika kila baada ya miaka miwili tangu kuanzishwa mwaka 2014, na mwaka huu umehudhuriwa pia na Rais wa Jamhuri ya Ghana, John Dramani Mahama.

Kwa upande wa Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.