Home KITAIFA CCM yaahidi ajira sekta ya elimu 7000 na afya 5000

CCM yaahidi ajira sekta ya elimu 7000 na afya 5000

Na Mwandishi wetu, Mwanza

MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema miongoni mwa mipango kazi ya miaka mitano ijayo, endapo chama hicho kitapewa tena ridhaa ya kushika dola ni pamoja na ongezeko la ajira mpya serikalini.

Amezitaja ajira hizo kuwa ni pamoja na ajira za walimu wa somo la hisabati na sayansi 7000 na ajira 5000 za kada ya afya.

Dk. Nchimbi ameyasema hayo Agosti 30, 2025,wakati akisalimiana na wakazi wa Kisesa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, akielekea viwanja vya Mwanankanda vilivyopo wilayani humo,kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo katika mkutano wa kampeni wa kukiombea chama hicho kura.

Amesema,mgombea Urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha miaka mitano ijayo akipewa ridhaa na wananchi,ndani ya siku 100 kati ya mambo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na mpango wa bima ya afya kwa wajawazito, watoto, walemavu na wazee na ongezeko la ajira serikalini.

“Yapo mambo mengi yaliyotekelezwa na Serikali kupitia ilani ya CCM na kwa kiasi kikubwa yamekamilika,”amesema Dkt.Nchimbi.

Pia Dk. Nchimbi amewaomba wakazi wa Kisesa kupigia kura ya ndiyo CCM,ili chama hicho kipate ridhaa ya kuongoza tena kwa kipindi kingine na kuendelea kuwaletea maendeleo.Huku akiwatoa hofu na kuwasihi kuendelea kuwa na imani na chama hicho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here