Home AFYA JKCI na SACH kufanya kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa...

JKCI na SACH kufanya kambi maalum ya upasuaji wa moyo kwa watoto 20 Zambia

Na Mwandishi wetu, Zambia

MADAKTARI Bingwa wa Upasuaji wa Moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto la nchini Israel (SACH) kufanya kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto 20 wa nchini Zambia.

Kambi hiyo ya siku sita inaanza leo Septemba, 8 2025 katika Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia (NHH) kwa kushirikiana na wataalamu wa Hospitali hiyo, na daktari wa usingizi kutoka nchini Ethiopia.

Akizungumza na mwandishi wa habari Septemba, 7 2025 nchini Zambia Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa JKCI Dk. Godwin Sharau alisema katika kambi hiyo utafanyika upasuaji wa kufungua kifua pamoja na upasuaji wa  tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

“Kambi hii inafanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nchini Tanzania, Zambia, Ethiopia, na Israel wote tukiwa na lengo la kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Zambia”, amesema Dk. Godwin

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel, Simon Fishers amesema Shirika hilo limeandaa kambi hiyo kuwasaidia wataalamu wa afya wa nchini Zambia na kuwajengea uwezo katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.

Amesema JKCI, na SACH wamekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 hivyo kupitia ushirikiano huo wamepanga kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Zambia.

“SACH imeweza kuwajengea uwezo madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI kwa kipindi cha muda mrefu, na baadaye kuanza kuwajengea uwezo wataalamu wa Hospitali ya Moyo Zambia hii yote ni kuhakikisha huduma bingwa bobezi za magonjwa ya moyo kwa watoto zinapatikana katika nchi hizi”, amesema Simon

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here