Na Florah Amon, Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, leo amezindua Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Ufugaji wa Nguruwe, linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia leo Septemba 11 hadi 13, 2025 linajulikana kama Tanzania Pig Expo 2025.

Pinda amesema kuwa kongamano hilo limekuja katika wakati muafaka ambapo sekta ya ufugaji wa nguruwe inatambulika kama kichocheo muhimu cha usalama wa chakula, lishe bora, ajira na ukuaji wa uchumi.
Amebainisha kuwa Tanzania imejaliwa mazingira bora ya kufanikisha sekta hii na inapaswa kuchangamkia fursa zilizopo kwa kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya uzalishaji.
“Ufugaji wa nguruwe si tu chanzo cha protini kwa Watanzania, bali pia ni lango la fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake hivyo ni vema mkafuga kwakuzingatia kanuni bora kwakuwapa lishe bora,” amesema Pinda.

Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 10 ya kaya nchini Tanzania zinajihusisha na ufugaji wa nguruwe, ambapo zaidi ya asilimia 90 ya nguruwe milioni 4.13 wanafugwa na wakulima wadogo wa vijijini kwa mifumo ya jadi nakusiisitiza haja ya kuwapa wakulima hao msaada wa kitaalamu, teknolojia, na masoko ili kuinua maisha yao.
Aidha kuwa pamoja na fursa hizo, pia Pinda amekiri kuwepo kwa changamoto zinazokabili sekta hiyo, zikiwemo magonjwa hatari kama homa ya nguruwe ya Afrika (ASF), gharama kubwa za chakula cha mifugo, uhaba wa mbegu bora na kutokuwepo kwa bima ya mifugo.
Ametoa wito kwa wadau wote wa sekta ya mifugo kushirikiana kwa vitendo kutatua changamoto hizo kwa kutumia tafiti, ubunifu na sera bora zinazolenga maendeleo ya mfugaji wa kawaida.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema kuwa sekta ya nguruwe ni eneo la kimkakati linalohitaji uwekezaji makini ili kufikia malengo ya Taifa ya kukuza uchumi shirikishi. Ameongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa kuboresha afya ya mifugo, upatikanaji wa malisho bora na mbegu zenye tija.
“Ongezeko la mahitaji ya nyama ya nguruwe katika miji na maeneo ya pembezoni ni fursa ya dhahabu kwa Tanzania. Tunahitaji kushirikiana kuimarisha mnyororo wa thamani, kutoka shambani hadi sokoni, kwa kutumia teknolojia na mbinu bora za kisasa,” amesema Katibu Mkuu.
Amesisitiza kuwa serikali inalenga kuanzisha vituo vya mfano vya ufugaji wa nguruwe katika kila kanda ili kutoa mafunzo na huduma za kibunifu kwa wafugaji amapo pia amewataka washiriki wa kongamano hilo kutumia jukwaa hilo kama nafasi ya kujifunza, kushirikiana maarifa na kubuni mikakati ya pamoja ya kuinua tasnia ya nguruwe barani Afrika.
Amebainisha kuwa serikali ya Tanzania iko tayari kuwa kitovu cha mageuzi ya sekta ya mifugo, hususan ufugaji wa nguruwe, kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa kwa jumla.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Nguruwe Tanzania (Tanzania Association of Pig Farmers – TAPIFA), Doreen Maro, amesema kuwa sekta ya ufugaji wa nguruwe nchini Tanzania inachangia kwa kiwango kikubwa lishe ya jamii, ajira kwa vijana na wanawake, na kipato cha wakulima wadogo.
“Zaidi ya asilimia 90 ya nguruwe nchini hufugwa na wakulima wadogo kwa njia za asili, hali inayowapa nafasi kubwa ya kunufaika iwapo kutakuwa na uwekezaji wa kimkakati katika mbegu bora, chakula cha bei nafuu, huduma za ugani, pamoja na masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi,” amesema Maro.
Kongamano la Kimataifa la Ufugaji wa Nguruwe, Tanzania Pig Expo 2025, linaendelea sambamba na mikakati ya taifa ya kuimarisha sekta ya mifugo kama kichocheo cha uchumi wa viwanda na kilimo biashara. Tanzania Pig Expo limekusanya wadau kutoka zaidi ya nchi 20 barani Afrika na duniani kote, na linafanyika chini ya kauli mbiu: “Ubunifu na Ukuaji katika Tasnia ya Nguruwe”.