Na Mwandishi wetu, Tanga
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha NLD, Doyo Hassan Doyo, akiwa safarini kuelekea Kiteto, Manyara, aliendelea na kampeni zake na kuwa hotubia wananchi wa Kijiji cha Kwediboma, Wilaya ya Kilindi, ambapo alieleza sera zake na mipango yake ya maendeleo endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na wakazi wa Kwediboma, Doyo alisema kuwa wananchi wa Kilindi wamesahaulika kimaendeleo kwa muda mrefu, hususan katika sekta za barabara, huduma ya maji safi, na afya. Aliongeza kuwa Kilindi hakuna barabara inayopitika kwa mwaka mzima ndani ya miaka 64 ya uhuru wa Tanzania, jambo linalowakwamisha wananchi kupata huduma muhimu ya kusafirisha mazao yao kwa wakati.
“Msingi wa maendeleo ni barabara. Wingi wa mazao mnayolima, ikiwemo mahindi na maharage, thamani yake inapotea kwa madalali kutokana na ukosefu wa barabara bora. Tukishapewa fursa ya kuongoza, tutajenga barabara hizi kwa kiwango cha zege kinachokidhi hali ya kijiografia ya mabonde ya eneo hili, hususan barabara ya Kilindi, Handeni,” amesema Doyo.
Aidha, ameibainisha kuwa amekutana na nyumba zilizobomolewa ili kurahisisha mradi wa ujenzi wa barabara, mradi ambao ulianza enzi za utawala wa Hayati Rais John Magufuli miaka minne iliyopita na bado wananchi hawajalipwa fidia. Mgombea huyo ameahidi kulipa fidia kwa wote walioguswa na bomoa, bomoa hiyo ili kufanikisha mradi huo.

Kwa upande wake, Meneja wa Kampeni wa mgombea huyo, Pogora Ibrahim Pogora, amesema kuwa Doyo ni kiongozi mzalendo anayezingatia haki na usawa. Aliongeza kuwa wananchi wa Kilindi wanapaswa kuzingatia changamoto zinazowakumba kila siku, ikiwemo barabara, maji na afya, na kumpigia kura Mhe. Doyo ili kuona thamani ya kura zao.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Kina Mama Taifa wa Chama Cha NLD, Saidati Fundi, alisema nchi hii, inahitaji mabadiliko ya kweli, na mabadiliko hayo yatapatikana kupitia Chama cha NLD.
“Tanzania haiwezi kupiga hatua ikiwa hatutakuwa na dhamira ya kumaliza matatizo yanayotokana na sera mbovu. Nchi inahitaji Viongozi wenye utashi, wananchi chagueni Viongozi wa chama cha NLD, Doyo ana dhamira ya kweli,”amesema.

Naye Muhamasishaji Mkuu wa Kampeni kwa upande wa kina mama, Adija Dikulumbali, aliwahimiza wanawake kutafakari kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo, hususan gharama za huduma za afya kwa wajawazito.
Ameongeza. “Thamani ya kura yenu ipo pale ambapo mtachagua kiongozi atakayewaletee maendeleo halisi. Mmesahaulika kwa muda mrefu, na sasa ni wakati wa kuibuka kidedea kwa thamani ya kura yenu.”
Msafara wa kampeni wa Doyo unaelekea Kiteto, Manyara, ambapo kampeni za kumnadi mgombea huyo zinaendelea, huku Chama Cha NLD kikijivunia hoja na sera zake zinazohamasisha usawa, uzalendo, haki na maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.