Home BIASHARA Dk. Mwinyi aahidi kudhibiti mfumuko wa bei na kuanzisha hifadhi ya mafuta...

Dk. Mwinyi aahidi kudhibiti mfumuko wa bei na kuanzisha hifadhi ya mafuta Zanzibar

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza katika uchaguzi mkuu ujao, kipaumbele chake kitakuwa kudhibiti mfumuko wa bei ya chakula na kuanzisha hifadhi ya mafuta ya dizeli na petroli, ili kudhibiti ongezeko holela la bei ya bidhaa hizo muhimu.

Akizungumza Jumamosi Septemba 13, 2025, katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa CCM uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, mjini Unguja, Dk. Mwinyi alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uchumi wa wananchi na kulinda maslahi ya taifa kwa ujumla, hasa nyakati za misukosuko ya kiuchumi duniani.

“Nchi za kimataifa zinapokuwa na migogoro ya vita, mara nyingi bei za mafuta hupanda kiholela. Ni jukumu letu kuwa na hifadhi itakayoweza kututosheleza angalau kwa zaidi ya miezi mitatu, ili wananchi wetu wasiguswe moja kwa moja na misukosuko hiyo,” alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa katika kipindi chake cha uongozi amesisitiza na kudumisha misingi ya amani, mshikamano na umoja wa Wazanzibari, akiondoa mambo yote ya ubaguzi, na sasa ni wakati wa kuelekeza nguvu zaidi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akitoa tathmini ya hali ya uchumi, Dk. Mwinyi alisema Zanzibar imeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.4, huku matarajio ya serikali yake ikiwa ni kufikia ukuaji wa asilimia 10 katika miaka michache ijayo. Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanakwenda sambamba na kuimarishwa kwa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu ya kijamii.

Kwa upande wa ajira, alisema serikali itahakikisha vijana wanapata nafasi zaidi kupitia sekta za viwanda, ajira za serikali pamoja na ujasiriamali, hatua itakayopunguza tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwao.

Katika uzinduzi huo, viongozi mbalimbali wa CCM walitoa salamu zao za hamasa. Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema Zanzibar ya sasa siyo ile ya miaka iliyopita, kwani imepiga hatua kubwa za kimaendeleo chini ya uongozi wa marais waliopita na sasa inaendelea kuimarika kupitia uongozi wa Dk. Mwinyi.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba, Dk. Mohamed Ali Shein, alisema kuwa Dk. Mwinyi ameonesha uongozi wenye dira na kusisitiza amani tangu aingie madarakani. “Nilimshuhudia tangu mwaka 2000 akiwa na nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi, na leo bado ameendelea kuwa kiongozi mwenye misimamo thabiti ya maendeleo na mshikamano. Zanzibar ikimchagua tena haitakuwa imebahatisha,” alisema Dk. Shein.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita, Amani Abeid Karume, aliwataka wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi kwa kujitokeza kupiga kura, akisisitiza umuhimu wa kutimiza wajibu wa kikatiba.

Uzinduzi huo wa kampeni ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja na viongozi wa CCM, huku shamrashamra mbalimbali zikifanyika kuashiria mwanzo rasmi wa mbio za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here