Na Mwandishi Wetu, Lajiji
Joto la Kariakoo Dabi linazidi kupanda kuelekea mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 16, 2025, ambapo watani wa jadi Yanga SC na Simba SC watakutana kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2025/26.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo, ametangaza orodha ya waamuzi watakaosimamia mchezo huo muhimu. Aidha, ameongeza kuwa waamuzi hao watakabidhiwa vifaa vya kazi kutoka kampuni ya JustFit, ambao pia wametangaza kutoa mipira maalumu kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hawa hapa waamuzi wa Kariakoo Dabi ya Septemba 16, 2025:
- Mwamuzi wa kati: Ahmed Arajiga
- Mwamuzi msaidizi namba 1: Mohamed Mkono
- Mwamuzi msaidizi namba 2: Kassim Mpanga
- Mwamuzi wa akiba: Ramadhani Kayoko
- Mtathmini wa waamuzi: Soud Abdi
Mara ya mwisho wababe hawa wawili kukutana ilikuwa Juni 25, 2025, katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambapo Yanga SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba SC. Hivyo basi, mchezo huu unatarajiwa kuwa kete ya kwanza ya msimu kwa watani hao wa jadi.