Na Esther Mnyika, Zanzibar
Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi wa visiwa hivyo kuendeleza jitihada za kudumisha amani, mshikamano na maridhiano, akisisitiza kuwa misingi hiyo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza, Septemba 18, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Amburu, Kaskazini Unguja, Dk. Mwinyi alisema hakuna taifa linaloweza kufanikisha maendeleo bila kuwepo kwa amani ya kudumu.
“Sera mama ya nchi yetu ni amani. Bila amani, hakuna maendeleo. Ndiyo maana tunapaswa kuiheshimu, kuilinda na kuikuza kwa vitendo,” alisema Dk. Mwinyi.
Tangu aingie madarakani mwaka 2020, Dk. Mwinyi amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia maridhiano ya kisiasa visiwani Zanzibar. Alibainisha kuwa utulivu na mshikamano ulioimarishwa kati ya wananchi licha ya tofauti za kisiasa, dini na kabila, umechangia kufanikisha miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo barabara, huduma za afya, elimu na uwekezaji wa kimataifa.
Dk. Mwinyi aliwaomba wawakilishi wa wananchi—akina mbunge, diwani na viongozi wa CCM—kuzingatia kuhubiri amani na mshikamano kila wanapopata nafasi ya kuzungumza katika majukwaa.
“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuwa balozi wa amani. Mnapopanda jukwaani, anzeni na kauli za mshikamano na maridhiano. Huu ndio msingi wa siasa safi na maendeleo ya kweli,” aliongeza.
Kauli hiyo imekuja wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikichukua kasi, huku wachambuzi wa siasa wakitafsiri wito wa Dk. Mwinyi kama njia ya kuimarisha misingi ya demokrasia Zanzibar, visiwa ambavyo kwa miaka mingi vimekumbwa na changamoto za kisiasa hasa nyakati za uchaguzi.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo waliuunga mkono wito wa Rais Mwinyi, wakisisitiza dhamira yao ya kushikamana na kulinda amani.
“Tumeona maendeleo makubwa chini ya uongozi wake. Tunaamini kuwa maridhiano na umoja ndivyo vitatupeleka mbali zaidi,” alisema Mwanaisha Haji, mkazi wa Mpendae.
Dk. Mwinyi anaingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais wa Zanzibar kwa kipindi cha pili, akibeba ajenda ya kuendeleza maendeleo, kuongeza ushirikishwaji wa wananchi, na kuimarisha zaidi misingi ya utawala bora na haki za binadamu.