Na Esther Mnyika, Zanzibar
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa endapo atachaguliwa kuongoza serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ukuaji wa uchumi wa Tanzania Bara unatarajiwa kufikia asilimia saba kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Akihutubia Septemba 18, 2025 katika Viwanja vya Amburu, Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Samia alisema matarajio hayo yanaendana na mafanikio ya Zanzibar ambapo kwa sasa uchumi wake unakua kwa kiwango hicho kutokana na utekelezaji wa sera bora za kifedha na kiuchumi.

“Sera za kiuchumi na kifedha zimefanya kazi nzuri zaidi. Tulikuwa tunakua kwa asilimia saba kabla ya Covid-19 na kuporomoka kwa uchumi, lakini Dk. Mwinyi ameweza kurudi haraka kwenye asilimia saba. Tuna matumaini kuwa mwaka 2026/27 tutarudi kwenye kiwango hicho pia kwa Bara,” alisema Dk. Samia.
Alibainisha kuwa changamoto za kiuchumi zilizoikumba Tanzania mwaka 2020 zilichangiwa na janga la Uviko-19, kuyumba kwa uchumi wa dunia na kupungua kwa misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo. Hata hivyo, ushirikiano kati ya serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar umewezesha kurejesha uthabiti wa kiuchumi.
Amesema kuwa utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali umesaidia kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta za afya, elimu, maji na miundombinu, hatua ambayo imeleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.
“Ukuaji huu sasa unamgusa mwananchi mmoja mmoja, jambo linaloonekana dhahiri kupitia ustawi na maendeleo ya kaya za Nungwi na maeneo mengine nchini,” ameongeza.