Na Esther Mnyika, Zanzibar
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali yake itaendeleza mpango wa mikopo isiyo na riba kwa ajili ya kuinua na kuwezesha biashara ndogo ndogo nchini.

Akizungumza Septemba 18, 2025, katika viwanja vya Amburu Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Samia alisema mpango huo utatekelezwa kwa pande zote mbili za Muungano ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa za kimaendeleo.
Alifafanua kuwa programu hiyo inalenga kuondoa changamoto zinazowakwamisha wajasiriamali wadogo na badala yake kuwawekea mazingira wezeshi ya kukuza kipato chao na kushiriki ipasavyo katika uchumi wa Taifa.
“Mikopo isiyo na riba hii nayo ni programu ya Tanzania nzima, na tunakwenda kuendelea nayo ili kunyanyua na kuwezesha biashara ndogo ndogo zikue. Wakati ninafungua kampeni kule Bara, suala moja nililosema ni kurasimisha biashara ndogo ndogo. Hii ni programu ya Muungano na tutakwenda kuifanya kwa pamoja, kurasimisha biashara ndogo ndogo kwa maana ya Tanzania Bara na hapa Zanzibar,” alisema.
Akizungumzia diplomasia, Dk. Samia alisema Tanzania imefanikiwa kuimarisha nafasi yake kimataifa kutokana na mshikamano wa pande mbili za Muungano.
“Suala la diplomasia, hili nalo ni suala la Muungano. Pande zetu mbili tumefanya kazi kwa pamoja na tumekuza uhusiano wa kidiplomasia, tumekuza jina la Taifa letu la Tanzania ulimwenguni. Sasa Tanzania iko vizuri na heshima tunayoipata ulimwenguni ni kwa sababu ya umoja na mshikamano wetu,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa mshikamano huo si tu umeliweka Taifa katika nafasi bora kimataifa, bali pia umefungua milango zaidi ya ushirikiano wa kimaendeleo na uwekezaji utakaonufaisha Watanzania wote.