Home BIASHARA Dk. Samia: TASAF umeondoa wengi katika umaskini, nitauendeleza

Dk. Samia: TASAF umeondoa wengi katika umaskini, nitauendeleza

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema usimamizi mzuri wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeleta matokeo makubwa kwa jamii, kwa kuwaondoa wananchi wengi kwenye kundi la umaskini na kuwawezesha kupata huduma za msingi.

Akizungumza Septemba 18, 2025 katika Viwanja vya Amburu, Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Samia alisema mfuko huo ni nguzo muhimu katika kupunguza changamoto za kimaisha kwa kaya maskini, na akaahidi kuendeleza usimamizi wake endapo atachaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Amesema, pamoja na kuimarisha TASAF, serikali yake pia itaendeleza mpango wa mikopo isiyo na riba ili kukuza biashara ndogo ndogo na kuwawezesha Watanzania kujiongezea kipato.

“Ndugu zangu, wakati ninafungua kampeni kule Tanzania Bara niliahidi kurasimisha biashara ndogo ndogo. Hili ni jambo la Muungano na tutakwenda kulifanya kwa pamoja — Bara na Zanzibar,” alisema Dk. Samia.

Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, alibainisha kuwa Tanzania imeimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kuendeleza ulinzi na usalama wa taifa, jambo lililoipa nchi heshima kimataifa.

“Mafanikio yote yanayoshuhudiwa na kusemwa kote nchini yametokana na tija ya kuenzi na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisisitiza, huku akiwataka Watanzania kuendelea kuulinda na kuuthamini.

Dk. Samia alisisitiza kuwa CCM, tofauti na vyama vingine, kinaona Muungano kama msingi wa ustawi na maendeleo ya taifa, akirejea kauli ya Mwalimu Julius Nyerere aliyouita Muungano huo “Lulu ya Afrika.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here