Home KITAIFA Dk. Mwinyi: Amani ya Zanzibar haitachezewa

Dk. Mwinyi: Amani ya Zanzibar haitachezewa

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa hataruhusu amani ya nchi ichezewe na mtu au kikundi chochote.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika, Septemba 22, 2025, katika Uwanja wa Shangani Mkoa wa Kaskazini A, Dk. Mwinyi alisema ataendelea kuhimiza mshikamano, maridhiano na umoja, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezekani bila amani.

“Maendeleo yoyote yanahitaji amani. Hatuko tayari kuona mtu yeyote anavuruga utulivu wa nchi. Amani ikidumishwa, tunafanya ibada na mikutano kama hii bila hofu. Atakayejaribu kuvuruga tutamdhibiti,” alisema.

Dk. Mwinyi alieleza mafanikio ya awamu ya nane katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na uchumi. Amesema serikali imeingia makubaliano na Kampuni ya NEC kutoka Oman kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji wa Dola milioni 26 utakaopunguza changamoto ya maji safi na salama Kaskazini Unguja.

Aidha, alisema utekelezaji wa mradi wa Bandari ya Manga Pwani na ujenzi wa kiwanja cha ndege utaibadilisha sura ya mkoa huo. Alibainisha pia kuwa zaidi ya Sh bilioni 96 zimetolewa kwa wananchi kupitia mikopo nafuu, sambamba na boti za kisasa kwa wavuvi ili kukuza uchumi wa buluu.

Amesema serikali itaendelea kuongeza maslahi ya wafanyakazi wa umma, kupandisha mishahara, posho na pensheni, huku sekta ya michezo ikipewa kipaumbele kwa kujenga viwanja kila wilaya.

Mwinyi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29 kwa mustakabali wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here