Home BIASHARA Dk. Mwinyi aahidi mikopo, mafunzo kwa wajasiriamali wa utalii Zanzibar

Dk. Mwinyi aahidi mikopo, mafunzo kwa wajasiriamali wa utalii Zanzibar

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameielekeza Taasisi ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZAEA) kuhakikisha wajasiriamali wanaopewa mikopo wanapatiwa pia mafunzo ya ujasiriamali ili kutumia fedha hizo kwa umakini na tija.

Akizungumza Septemba 22, 2025 na vijana wa sekta ya utalii Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa wajasiriamali na kuwatengea maeneo maalumu ya kuuzia bidhaa zao hususan beach boys na beach girls.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa sekta ya utalii inachangia asilimia 30 ya pato la Zanzibar, na kuongeza kuwa watalii wanahitaji mambo matatu: usalama, fukwe safi na nzuri, pamoja na kuheshimu utamaduni.

“Kila atakayepokea mkopo lazima apate mafunzo ya ujasiriamali. Serikali pia itatoa mitaji na mikopo isiyo na riba kuhakikisha vijana wa utalii wanainuka kiuchumi. Polisi wa utalii kazi yao ni kulinda usalama, siyo kupiga watu. Rushwa na unyanyasaji nitakomesha,” alisema.

Baadhi ya beach boys na beach girls walimshukuru kwa kusikiliza changamoto zao, wakisema wamekuwa wakibaguliwa, kutozwa kodi kubwa na wakati mwingine kunyanyaswa.

Kwa upande wake, Khadija Kombo Mussa, anayejishughulisha na huduma za massage, alisema wanahitaji amani na mazingira bora ya kufanya biashara ili kuendeleza sekta ya utalii kwa manufaa ya wote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here