Home BIASHARA Dk. Mwinyi: Amani, umoja na maridhiano ndiyo nguzo za maendeleo Zanzibar

Dk. Mwinyi: Amani, umoja na maridhiano ndiyo nguzo za maendeleo Zanzibar

Na Esther Mnyika, Zanzibar

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa sasa wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuendeleza juhudi za kudumisha amani, mshikamano na maridhiano, akisisitiza kuwa hayo ndiyo misingi ya maendeleo ya taifa.

Akihutubia wananchi katika Viwanja vya Amburu, Kaskazini Unguja leo Septemba 18, 2025, Dkt. Mwinyi alisema hakuna taifa duniani linaloweza kusonga mbele bila kuwa na amani ya kudumu.

“Sera mama ya nchi yetu ni amani. Bila amani, hakuna maendeleo. Ndiyo maana tunapaswa kuiheshimu, kuilinda na kuikuza kwa vitendo,” alisema.

Alibainisha kuwa tangu aingie madarakani mwaka 2020, amekuwa mstari wa mbele kusimamia maridhiano ya kisiasa na mshikamano wa kijamii, hali iliyochangia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miundombinu, afya, elimu na uwekezaji.

Dkt. Mwinyi aliwataka wabunge, madiwani na viongozi wa CCM kutumia majukwaa ya kisiasa kuhimiza maadili ya amani na mshikamano. “Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuwa balozi wa amani. Huu ndio msingi wa siasa safi na maendeleo ya kweli,” alisema.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionyesha kuunga mkono wito huo, wakisema umoja na maridhiano ndiyo nguzo zitakazoipeleka Zanzibar mbele.

Dkt. Mwinyi anaingia kwenye kinyang’anyiro cha pili cha urais akiahidi kuendeleza ajenda ya maendeleo, mshikamano wa kitaifa na kuimarisha utawala bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here