Na Mwandishi wetu, Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo akipewa ridhaa ya kuongoza tena atahakikisha anaboresha masoko ya wafanyabiashara ili kuona wafanyabiashara katika mazingira mazuri.

Akizungumza leo Septemba 29 2025 kwa wajasiriamali wa soko la Mwanakwerekwe ikiwa ni muendelezo wa kampeni za kuomba kura, Dk.Mwinyi amesema, katika uongozi wake atahakikisha masoko mengine anajenga ikiwemo la Kwahajitumbo, Fuoni, Kibandamaiti, Kisauni.
Amesema, serikali yake imeahidi kuwaweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara hivyo ahadi yake ataendeleza kwa makundi mbalimbali.

Hata hivyo, amesema kipindi kilichopita wametoa shilingi bilioni 96 kwa wajasiriamali mbalimbali hivyo aliahidi kwa mwaka huu kuengeza fedha ili kuweza kukidhi kwa wafanyabiashara.
Amewaahidi kuendelea kuziondoa changamoto zinazowakabili wajasiriamali ikiwemo vibaraza vya kufanyia biashara.

“Kwa sasa mumekuwa mukitoa shilingi 30 za kodi na elfu 10 za usafi hivyo kwa mwezi munatoa 40 basi tutahakikisha tunaweka bei iliyokuwa nzuri zaidi ili muweze kuimudu,”amesema.
Amewataka wajasiriamali hao ifikapo Oktoba 29 kumchagua tena ili aendeleze kuwa Rais wa Zanzibar na Dk.Samia Suluhu Hassan na viongozi wa chama hicho ili kuendeleza maendeleo kwa wananchi.