Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
WADAU wametakiwa kuendelea kushirikiana na jamii kupaza sauti kwa pamoja ili kutokomeza ukatili wa kijinsia unaoendelea kuwa tatizo sugu katika jamii, na matukio yake yamekuwa yakiongezeka na kujirudia mara kwa mara nchini

Wito huo umetolewa Septemba 30, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben, wakati wa mafunzo yaliyofanyika chini ya mradi uitwao ‘Sauti Zetu’ unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya TAMWA na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Amesema ukatili wa kijinsia umekuwa sugu katika familia na kila kundi linaathirika na ukatili huo miongoni mwa waathirika wakubwa ni watoto, wanawake na makundi mengine.
“TAMWA peke yake haiwezi kukomesha tatizo hilo bila ushirikiano kutoka kwa jamii, serikali na wadau mbalimbali hivyo ni lazima jamii nzima ishiriki kupaza sauti ili kuleta suluhisho la kweli kwa janga hili la ukatili wa kijinsia,” amesema

Amefafanua kuwa, ukatili wa kisaikolojia unaonekana kuwa mkubwa zaidi, kwani mtu anapoumizwa kisaikolojia anaweza kuwa chanzo cha kufanya ukatili mwingine katika jamii.
Dk. Rose amesema lengo la mafunzo hayo ni kuiwezesha jamii kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu ukatili wa kijinsia na kupaza sauti dhidi ya vitendo hivyo.
“Tumejumuisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kina mama kutoka masokoni, maafisa wa serikali kutoka ngazi mbalimbali, na waandishi wa habari kwa lengo la kujadili namna bora ya kukomesha ukatili huu,” amesema Dkt. Reuben.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo walitoa shuhuda mbalimbali katika mafunzo hayo, Mwalimu Annamaria Ngawambala wa Shule ya Sekondari Mugabe amesema ukatili wa kijinsia kwa watoto bado ni changamoto kubwa, hasa kwa familia zenye hali duni ya kiuchumi na utengano wa wazazi.

“Mtoto anakosa mahitaji ya msingi, haendi shule anakuwa kujishughulisha na biashara kuna muda anakuwa mwanafunzi wakati mzazi katika umri mdogo. Utengano wa wazazi huathiri malezi, huku walimu wakibeba jukumu la kulea watoto pekee yao,” amesema.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walieleza aina ya ukatili wanaokutana nao, kama vile lugha za matusi kutoka kwa makonda wa daladala na kejeli kutoka kwa walimu wawapo shuleni.
“Unakuta unataka kupanda daladala, konda anakusukuma au hakurudishii chenji. Shuleni, ukikosea kujibu swali, mwalimu anakutukana na wenzako wanakucheka,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIKI, Janeth Mawinza, amesema taasisi hiyo inashughulika na chanzo cha ukatili wa kingono kwa lengo la kuzuia vitendo hivyo.
Ameeleza kuwa wameanzisha kampeni ya Safari Salama bila rushwa ya ngono kwa wasichana, ambapo wanatembelea shule mbalimbali na vituo vya bodaboda kutoa elimu kwa wanafunzi na vijana.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Kituo cha Mkono kwa Mkono Mwananyamala, Halili Katani, alisema kuwa serikali inaendelea kulishughulikia tatizo hilo kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa wahanga wanapata huduma stahiki kwa wakati.

“Wahanga wa ukatili wanapaswa kupata huduma kutoka kwa polisi, wahudumu wa afya, maofisa ustawi na watoa huduma wengine mahali pamoja,” amesema Katani.