Home SIASA Hatutokubali katiba ivunjwe kwa makelele ya mitandaoni-Makonda

Hatutokubali katiba ivunjwe kwa makelele ya mitandaoni-Makonda

Na Mwandishi wetu, Mwanza

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda leo Jumanne Oktoba 07, 2025 akiwa Nyamagana Mkoani Mwanza kwenye Kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Dk. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa kama wanachama wa Chama hicho hawatokubali kumuona Dk. Samia anavunja Katiba ya Tanzania kutokana na kile alichokiita “Makelele ya Mtandaoni.”

Makonda kwenye Mkutano huo wa Kampeni unaofanyika kwenye Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana amesisitiza kuwa Tanzania imeundwa kwenye misingi imara, akibainisha kuwa uchaguzi ni suala la Kikatiba na sio matakwa ama hisia za mtu binafsi na kamwe nchi haiwezi kuendeshwa kwa matamko bali kwa kuzingatia Katiba ambayo Dk. Samia aliapa kuilinda wakati anachukua madaraka.

Amewataka watanzania pia kutokubali kushawishiwa na kushiriki kwenye kuvuruga amani ya Tanzania, akiwakumbusha Vijana kuwa wanaochochea uvunjifu wa amani ya Tanzania ni watu ambao hawapo ndani ya Tanzania na hata waliopo tayari wanazo pasi zao za kusafiria ikiwa nchi itaingia kwenye ukosefu wa amani na vurugu.

“Dk. Samia wakati alipoondoka duniani Hayati Dk. John Pombe Magufuli, aliapa kuilinda katiba na sisi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi hatutakubali aivunje Katiba kwa kuruhusu kelele za kwenye Mitandao. Na wengi wanaofanya uchochezi ukiwatazama wana passport na wengine hawapo nchini niwaombe sisi tulioko hapa na tulioona kazi njema iliyofanywa na Dk. Samia tuendelee kumuunga Mkono,” amesisitiza Makonda.

Makonda ametumia sehemu ya salamu zake pia mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza Dk. Samia, kufanya maombi maalumu ya kula agano na wananchi hao katika kumuunga Mkono Dk. Samia na kutotumia mikono yao kutenda matendo yanayohatarisha amani ya Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla kuelekea uchaguzi Mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here