Home AFYA MOI,JWTZ na Jeshi la Ulinzi la Misri kushirikiana kutoa huduma za kibingwa...

MOI,JWTZ na Jeshi la Ulinzi la Misri kushirikiana kutoa huduma za kibingwa na kibobezi

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Ulinzi la Misri kushirikiana katika kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 7, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya wakati wa mazungumzo ya ushirikiano kati ya taasisi hizo tatu.

Kupitia ushirikiano huo, wataalamu kutoka Tanzania na Misri watashirikiana katika maeneo ya upasuaji wa kibingwa na kibobezi na magonjwa ya ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu na Mifupa.

Ushirikiano huo pia unalenga kupanua wigo wa ushirikiano na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kupitia mafunzo ya vitendo (seti) warsha na kubadilishiana uzoefu wa kitaaluma.

Akizungumza katika kikao hicho cha ushirikiano Dk. Mpoki amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya nchini Tanzania hususani za kibingwa na kibobezi za mifupa na ubongo.

“Kupitia ushirikiano huu, tunalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kibingwa, kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi” amesema Dk. Mpoki na kuongeza kuwa

“Zaidi ya asilimia 98 ya wagonjwa wa mifupa wanatibiwa nchini Tanzania kupitia taasisi yetu ya MOI na asilimia 97 ya wagonjwa wa ubongo na mishipa ya fahamu wanatibiwa nchini”

Kwa upande wake Kiongozi mkuu wa msafara kutoka Jeshi la Misri Meja Jenerali Wael Abdallah Mohamed Aly aliyeambatana na timu ya madaktari kutoka Misri na Brigedia Jenerali AM Katua ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Tiba cha Jeshi (JETTZ), amesema amefurahishwa na huduma za kibingwa na kibobezi zinazotolewa na MOI na anaamini kupitia ushirikiano huo utaleta matokeo chanya katika nyanja ya afya baina ya pande zote tatu.

“Nimefurahi kuwa nanyi hapa leo, ushirikiano huu ni muhimu kwa pande zote kwa maana wataalam wetu na wenu wataweza kukutana na kubadilishana uzoefu,” Meja Jenerali Wael.

Ushirikiano huu unalenga kuongeza ufanisi katika utoaji huduma na kubadilishana uzoefu miongoni kwa Taasisi hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here