Home KITAIFA Mgombea ubunge wa CUF auawa Kilimanjaro

Mgombea ubunge wa CUF auawa Kilimanjaro

Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro

JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu 8 kwa tuhuma za mauaji ya Daudi Wilbard Ntuyehabi, aliyekuwa ni mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) katika jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mauaji hayo yametokea jana Oktoba 7 2025 majira ya saa 1:30 usiku katika kijiji cha Kilingi Sanya juu wilaya ya Siha mkoani humo.

“Tukio la kujichukulia sheria mkononi limetokea baada ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu) kumchoma kwa kisu tumboni Abdul Issa Mohamed mkazi wa Kilingi kata ya Sanya Juu na kusababisha utumbo kutoka nje”. Taarifa ya polisi imesema.

“Inadaiwa sababu zilizopelekea Abdul Issa Mohamed kuchomwa kwa kisu ni ni kitendo chake cha kwenda kuamua ugomvi uliozuka kati ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu)na Hamadi Issa Mohamed wakati wanakunywa pombe kwenye grocery kutokana na kudaiana fedha.” Imeongeza taarifa ya polisi.

Kufuatia tukio hilo watu hao nane walimshambulia Daudi Wilbard Ntuyehabi, kitendo ambacho ni kujichukulia swheria mkononi na kumsababishia kifo. Watuhumiwa hao ni pamoja na Hamadi Issa Mohamed, Alphonce Kinyaha, Rizik Amedeus, Frank Paulo Lutindi na Shedrack Emanuel. Wengine ni Jeremiah Mnkondo, Zainab Elisha na Issah Mohamed.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Abdul Issa Mohamed bado anapatiwa matibabu hospitalini. Kufuatia tukio hilo jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutojichukulia sheria mkononi kutokana na madhara makubwa yanayotokea baada ya wao kufanya hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here