Na Mwandishi wetu, Tabora
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, imemhukumu mkulima na mkazi wa Kata ya Mbagwa wilayani humo, Boniface Matale (30) kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti kijana mwenzake mwenye matatizo ya akili.

Hukumu hiyo imetolewa Oktoba,8 2025 na Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Nzega, Nasra Mkadam na kusema ametoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Amesema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa mbele ya mahakama hiyo na usiotia shaka yoyote, hivyo imeridhia Boniface Matale aitumikie adhabu ya miaka 30 jela.
Hakimu Nasra amesema adhabu hiyo itakuwa fundisho kwake na watu wengine wenye nia ya kufanya vitendo hivyo vya kikatili kwa watu wenye matatizo ya akili kama kijana huyo.
Nasra aliendelea kuiambia mahakama hiyo kwa kusema kwamba vitendo vya ukatili vya ubakaji na ulawiti vimekuwa vikitokea mara kwa mara kwenye Wilaya ya Nzega na adhabu hizo zitakuwa ni fundisho kwa wengine.
Awali, Wakili wa Serikali, Enock Kigolya aliieleza mahakama hiyo kwamba Agosti 19, 2025 majira ya usiku katika Kata ya Mbagwa nyumbani kwa kijana huyo, Matale aliingia na kumlawiti.
Amesema kitendo hicho kilishuhudiwa na dada wa kijana huyo mwenye matatizo ya akili ambaye hata kuzungumza hawezi kutokana na matatizo hayo ya akili.
Mshitakiwa huyo aliomba kupunguziwa adhabu kwa kuwa ana umri mdogo na anategemewa na wazazi wake.