Home KITAIFA Ujenzi wa kiwanja cha ndege Msalato umefikia asilimia 95 miundombinu asilimia 63

Ujenzi wa kiwanja cha ndege Msalato umefikia asilimia 95 miundombinu asilimia 63

Na Mwandishi wetu, Dodoma

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma umeendelea na utekelezaji wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambapo hadi hivi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 95.95 sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na asilimia 63 sehemu ya ujenzi wa majengo.

Hayo yameelezwa Oktoba 10 2025 na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi katika Kiwanja cha Ndege hicho.

“Utekelezaji wa mradi huu unaendelea vizuri ambapo Kwa upande wa miundombinu umefikia asilimia 95.95 na kwa upande wa majengo umefikia asilimia 63”, ameeleza Mhandisi Zuhura.

Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa sehemu ya ujenzi wa majengo unahusisha jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia watu (1,500,000), Mnara wa kuongozea ndege, pamoja na majengo ya huduma za dharura kama Zimamoto na Hali ya hewa.

Amebainisha kuwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu unahusisha barabara za maingilio, barabara za kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, mifumo ya maji safi na maji taka, uzio pamoja na taa za kuongozea ndege.

Aidha, Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo kwa sehemu zote mbili unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 360.

Pia amesema utekelezaji wa Kiwanja hicho utazingatia viwango vya Kimataifa ambapo utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa zenye abiria zaidi ya 300 huku ukiwa na maegesho ya magari 500 kwa wakati mmoja.

Vilevile, Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa mradi huo umeleta manufaa ya kiuchumi kwa wakazi wa Dodoma kwani umeweza kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 2,000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here