π Dk. Biteko ataka utekelezaji wa kuleta matokeo chanya
π Mradi kugharimu Dola za Kimarekani milioni 38.7
π WHO, FAO, UNICEF na Pandemic Fund zaipongeza Tanzania
Na Mwandishi wetu, Mwanza
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amezindua Mradi wa Dunia wa kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko nchini na kuzitaka wizara zote tawala za mikoa na serikali za mitaa pamoja na taasisi kutekeleza shughuli za kipaumbele katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na dharura za kiafya.

Dk. Biteko ametoa agizo hilo Oktoba 15, 2025 jijini Mwanza na kusema mradi huo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 38.7 unalenga kuboresha huduma za afya kwa watanzania na kuchochea maendeleo ya nchi.
Amesisitiza kuwa wizara, taasisi na washirika wa maendeleo wanatakiwa kusimamia utekelezaji katika uwekezaji huo na kuhakikisha yanapatikana matokeo chanya kama ilivyokusudiwa.
βWizara zote, Tawala za mikoa na Taasisi , tekelezeni shughuli zote za kipaumbele katika kukabiliana na magonjwa haya ya mlipuko na dharura nyingine za afya kulingana na maeneo yenu na hakikisha kwamba hakuna hata shilingi moja inayopotea au kuchepushwa kando ya malengo yaliyokusudiwa,β amesema Dk. Biteko.

Amesema kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na wadau wote wa ndani na nje ya nchi kuimairsha mradi huo ili uweze kuleta matokeo chanya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa tishio kwa maisha ya watu na kurudisha nyuma maendeleo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema uzinduzi wa mradi huo, ni muhimu katika jitihaza za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Amesema mradi huo unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia sehemu ya Afya moja pamoja na wadau wa maendeleo likiwemo Shirika la Afya Duniani(WHO), Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Pandemic Fund.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Magembe amesema mradi huo utaboresha mwitikio wa mifumo ya afya katika kukabiliana na magonjwa kama Ebola, MPOX, Marburg, ZIKA na magonjwa mengine yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amefafanua kuwa utekelezaji madhubuti utawezesha upatikanaji wa taarifa za haraka kuhusu uwepo au uvumi kuhusu magonjwa ya mlipuko na hivyo kuzifanyia kazi taarifa hizo.
Amesema upatikanaji wa fedha hizo utawezesha pia maboresho ya maabara ya taifa na kikanda ikiwa ni njia ya kupata taarifa za haraka kwa usahihi kutoka kwa wananchi.
Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Salim Nassor Slim amewashukuru viongozi wa Kitaifa kwa hatua za kuboresha afya za wananchi ili kuwa na afya bora.
Naye Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Dk. Patricia Safi ameipongeza Tanzania kwa ushirikiano ulipo kati yake na mashirika ya kimataifa na kuongeza kuwa Shirika hilo litahakikisha linaendeleza mashirikiano katika kutatua changamoto za kijamii.
Amesema UNICEF itahakikisha mchango wake unajikita katika maendeleo ya mtoto na kufanya jitihada za kuwezesha watoto wote wanapata huduma kwa mujibu wa mipango iliyopo.