Home SIASA Dk. Mwinyi aahidi nafasi zaidi za uongozi kwa watu wenye ulemavu...

Dk. Mwinyi aahidi nafasi zaidi za uongozi kwa watu wenye ulemavu Zanzibar

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuimarisha uwezeshaji wa watu wenye ulemavu kiuchumi kupitia ajira, elimu, na upatikanaji wa vifaa saidizi endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuiongoza Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano maalum na watu wenye mahitaji maalum uliofanyika leo, Oktoba 15, 2025, katika Ukumbi wa Idrisa Abdulwakil, Kikwajuni, Dk. Mwinyi amesema serikali yake itatoa mazingatio maalumu kwa watu wenye ulemavu katika ajira za umma, uongozi, na elimu ya amali.

Amebainisha kuwa serikali itahakikisha idadi ya watu wenye ulemavu inaongezeka katika vyombo vya utungaji wa sheria, na vilevile katika nafasi za uongozi serikalini.

“Kwenye vyombo vya utungaji wa sheria tutahakikisha kuna idadi kubwa na nzuri zaidi ya watu wenye ulemavu. Hata kwenye nafasi za uongozi ambazo mimi ninateua, nitahakikisha kundi lao linakuwa kubwa zaidi,” amesisitiza.

Akizungumzia sekta ya elimu, Dk. Mwinyi amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watu wenye ulemavu, hasa kupitia vyuo vya amali vinavyotoa mafunzo ya ufundi na ujasiriamali.

Kwa upande wa upatikanaji wa vifaa saidizi, Dkt. Mwinyi ameahidi kwamba serikali itaendelea kugharamia vifaa hivyo kwa watu wenye ulemavu bila malipo, huku ikipunguza gharama kwa wauzaji binafsi.

“Serikali itaendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu kupata vifaa hivi saidizi bila ya malipo. Kwa wale wanaouza katika maduka binafsi, serikali itaondoa ushuru ili bei zishuke,” amefafanua.

Amesisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu linapata nafasi sawa na makundi mengine katika kujiletea maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here