Home UCHUMI BoT yakanusha kuchapisha fedha kwa ajili ya uchaguzi

BoT yakanusha kuchapisha fedha kwa ajili ya uchaguzi

Na Mwandishi wetu

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imekanusha uvumi wa taarifa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa imechapisha na kusambaza fedha kwa ajili ya kugharamia uchaguzi mkuu.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Tutuba, BoT imesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakihamasishwa kuondoa fedha zao kwenye benki za biashara kwa madai kuwa zinaishiwa fedha kutokana na uchaguzi, madai ambayo imesema hayana ukweli wowote, ni upotoshaji unaolenga kupotosha umma.

Licha ya BoT kusisitiza kuwa taarifa hizo ni za uongo na zinapaswa kupuuzwa na umma, kupitia taarifa hiyo imetoa uffanuzi kuwa, kuchapisha fedha hufanywa kwa mujibu wa sheria kama ilivyo katika nchi nchingine duniani.

“Benki Kuu ya Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, huchapisha fedha kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura ya 197, Benki Kuu ina jukumu la kuzungusha kiasi cha fedha kinachohitajika katika shughuli za kiuchumi pamoja na mahitaji ya kubadilisha fedha zilizochakaa pale zinaporejeshwa benki kuu kupitia amana za benki za biashara na siyo vinginevyo” taarifa hiyo imedokeza.

kufuatia upotoshaji huo, BoT imewaomba wananchi kutohamisha fedha zao kutoka kwenye mabenki bali waendelee kutumia huduma za benki bila wasiwasi wowote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here