Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WADAU kutoka serikalini, mashirika ya kiraia na wakulima wamekutana mkoani Morogoro kujadiliana kuhusu nafasi ya mbegu za wakulima kwenye Itifaki ya Eneo Huru la Biashara Africa (AfCFTA).

Akifungua mkutano huo Mratibu wa Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi, itifaki hiyo ambayo Tanzania imesaini inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, hivyo wao kama wadau wameona ni muhimu kujadiliana ili kuangalia hatma ya mbegu za wakulima.
Amesema takwimu zinaonesha asilimia 70 ya mbegu zinazotumika kwenye kilimo Afrika zinatoka kwa wakulima, hivyo imani yao ni kuona zinaendelea kupewa kipaumbele, ili itifaki hiyo isije kuziathiri.
“Mkutano huu wa siku moja umekutanisha wadau kutoka Wizara ya Kilimo, Viwanda na Biashara, mashirika ya kirai yanayopigania kilimo ikolojia, wakulima na makundi mengi, kujadili itifaki ya AfCFTA ambayo imekuja kufungua fursa za masoko barani Afrka,”amesema.
Mkindi amesema itifaki hiyo inaweza kuwa na athari hasi na chanya ambapo alibainisha kuwa mbegu nyingi za wakulima hazitambuliki kisheria, hivyo zinaweza zisiingie kwenye mfumo wa biashara huru ambao unatambulika duniani kote.

Akizungumzia juu ya itifaki hiyo kuwa na matokeo chanya ni pale ambapo serikali itatambua mbegu za wakulima kisheria, hivyo wakulima watapata fursa za kuuza kwenye soko la Afrika.
Naye Mtafiti na Mchechemuzi Kilimo Ikolojia wa TABIO, David Manongi amesema kikao hicho kinatoa fursa kwa wadau kujadiliana juu ya bishara huru Afrika, ili kuwezesha wakulima kunufaika na fursa zilizopo.
Amesema mijadala hiyo kuhusu itifaki ya AfCFTA inachangia kutoa msukumo kwa serikali za Afrika kuweka mikakati, kujipanga na kulinda haki za wakulima wadogo.
“Lakini pia hakuna sera maalum iliyopo juu ya umiliki unaonesha moja kwa moja uzalishaji wa nasaba muhimu kama vitunguu vya Mang’ula, Mchele wa Kyela, Kamsamba na nyingine,” amesema.
Manongi amesema ni wajibu wa serikali kuyalinda maeneo yenye nasaba za mimea zilizotambuliwa kisheria hasa kupitia Mkataba wa Kimataifa kuhusu Rasilimali za Kijenetiki za Mimea kwa Ajili ya Chakula na Kilimo (ITPGRFA) ambayo tumesaini.
“Tulianza mchakato wa kutengeneza sheria ya kulinda nasaba za mimea tangu 2008, ila bado haijakamilika na kwamba ni muhimu kulinda nasaba za mimea kupitia sheria,” amesema.
Amesema TABIO kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo ikolojia wamefanikiwa kuanzisha benki za mbegu 48 nchini kote ambazo zimegawanywa kwenye kanda.
Aidha, mtafiti huyo ametoa ombi kwa serikali na wadau wengine kuomba nasaba za mimea ambazo zimehifadhiwa kwenye benki ya mbegu duniani.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Abdulkarim Nzori amesema AfCFTA inalenga kuwa na soko moja la biashara barani Afrika, kwa kuhakikisha inaondoa vikwazo mbalimbali vya biashara.
Ameongeza kuwa AfCFTA katika kufanikisha adhma hiyo pamoja na mambo mengine ilianzisha mchakato wa kupata Itifaki itakayosimamia Haki za Miliki Ubunifu barani Afrika. Hivyo, majadiliano ya Itifaki ya Miliki Ubunifu chini ya AfCFTA yalianza kwa mara ya kwanza mwaka 2022 na 2023 ilipitishwa na kuanza kutekelezwa hasa kwa kuboresha mazingira ya biashara Afrika kuwa rafiki na haki za miliki ubunifu kushabihiana na nchi zingine.
“Ibara ya 40 na 41 ya itifaki hii imetoa fursa kwa Nchi Wanachama kuanza kujadili viambatisho muhimu vya Haki za Miliki Ubunifu kama vile Alama, Hataza, Maumbo, Ulinzi wa Mbegu Mpya za Mimea, Viashiria vya kijiografia na viambatisho vingine ambapo kwa sasa viambatisho hivyo vipo kwenye hatua mbalimbali za maamuzi na matarajio yetu muafaka utafikiwa,” amesema.
Nzori amesema itifaki hii inawataka nchi wanachama kuwa na sheria zitakazotambua haki za mkulima, ulinzi wa mbegu na ulinzi wa viashiria vya kijiografia. Hili linatoa fursa kwa Tanzania kama nchi mwanachama kuweza kulinda bidhaa mbalimbali kama vile mchele wa Kyela, Kamsamba na bidhaa nyingine kama viashiria vya kijiografia.
Amesema itifaki hii inachochea ubunifu, shughuli za viwandani, kusafirisha teknolojia na kurahisisha uhamishaji wa bidhaa kwa nchi za Afrika.
Mtaribu Msaidizi Kitengo cha Jinsia na Maendeleo, Jimbo Katoliki Mbulu mkoani Manyara, Winfrida Patrick alisema ujio wa itifaki huu unapaswa kuzingatia ulinzi wa mbegu za wakulima kwani dalili zinaonesha kushuka.
Winfrida amesema jimbo hilo linafanya kazi na vikundi 14 vya wakulima katika Wilaya ya Mbulu na Babati, hivyo wameanza kuona changamoto baada ya itifaki hiyo kuanza kutekelezwa.
“Sisi tuna vikundi 14 vya wakulima ambavyo vinajihusisha na kilimo cha mbegu asili ambazo zina manufaa kiafya, kimazingira na kijamii kutokana na virutubishi vilivyo,” amesema.
Mkulima Salvatory Katembwa kutoka kijiji cha Usoche Kamsamba wilayani Momba mkoani Songwe amesema amejikita katika kilimo cha mbegu asili kwa kuwa haina madhara kwa binadamu.
“Kilimo cha asili ni kizuri kwa kuwa hakitumii mbolea za kemikali, sisi tunatumia mboji na takataka ambazo hazijapita kiwanda. Naomba nitumie nafasi hii kuiomba serikali itoe elimu umuhimu wa kutumia mbegu za asili,” amesema.
Katembwa amesema mbegu asili zinazaa kiwango ambacho kinaridhisha na soko la mazao yanayozingatia kilimi ikolojia ni la uhakika.
“Mimi nalima mchele ambao ni asili, situmii mbolea ya kemikali, natumia mboji na zingine za asili, lakini mchele huo una harufu nzuri na faida ya kibiashara ni nzuri,” amesema.