Home KITAIFA Darasa la nne kufanya mtihani wa mtaala mpya kesho

Darasa la nne kufanya mtihani wa mtaala mpya kesho

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

JUMLA ya wanafunzi 1,582,140 kutoka shule 20,517 zilizopo Tanzania Bara wamesajiliwa kushiriki katika Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utakaofanyika l kesho kwa kuzingatia sera mpya ya elimu ya mwaka 2014 toleo 2023 na mtaala ulioboreshwa.

Kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 764,290 sawa na asilimia 48.31, huku wasichana wakiwa 817,850, wakichangia asilimia 51.69 ya jumla ya watahiniwa, hali inayoonesha ushiriki mkubwa wa watoto wa kike katika elimu ya msingi.

Akizungumza leo Oktoba, 21 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed alisema wanafunzi 1,475,637 sawa na asilimia 93.27 watafanya upimaji kwa lugha ya Kiswahili.

Amesema wanafunzi106,503 sawa na asilimia 6.73 wakifanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo imekuwa lugha ya kujifunzia katika shule zao.

“Upimaji huu pia umezingatia kundi la wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo jumla ya wanafunzi 5,750 wamesajiliwa. Kati yao, 1,164 wana uoni hafifu, 111 ni wasioona, 1,161 ni wenye uziwi, 1,641 wana ulemavu wa akili na 1,673 wana ulemavu wa viungo.

“Mwaka huu wanafunzi wa Darasa la Nne watafanya mitihani kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya 2014 toleo la 2023 pamoja na mtaala ulioboreshwa, ikiwa ni hatua muhimu katika maboresho ya elimu nchini,” amesema.

Amesema masomo yatakayopimwa ni sita ya lazima ambayo Sayansi, Hisabati, Jiografia na Mazingira, Sanaa na Michezo, Kiswahili, English Language, pamoja na Historia ya Tanzania na Maadili lakini kutakuwa na somo moja la kuchagua kati ya Kifaransa, Kiarabu au Kichina.

Profesa Mohamed ameeleza kuwa lengo kuu la upimaji huo ni kupima kiwango cha uelewa wa wanafunzi katika stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, pamoja na umahiri wao katika masomo husika ili kuimarisha ubora wa elimu nchini.

Amesema maandalizi yote ya upimaji huo yamekamilika, ikiwa ni usambazaji wa karatasi za mitihani na nyaraka zote muhimu katika halmashauri zote. Vilevile, maandalizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum yamefanyika kikamilifu.

Katibu huyo alizitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama na utulivu katika vituo vyote vya mitihani.

“Tunawakumbusha wasimamizi kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na kuzingatia miongozo waliyopewa na wanafunzi wenye mahitaji maalum tumewapa muda wa ziada kuhakikisha wanapata fursa sawa katika upimaji huo,” amesema.

Kwa wanafunzi, NECTA ilieleza kuwa inatarajia watatekeleza maadili ya mtihani kwa kufuata kanuni zote na kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na udanganyifu atafutiwa matokeo kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Vilevile wamiliki wa shule na wakuu wa shule wameaswa kutokuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani hivyo wanakumbushwa kuwa shule ni vituo rasmi vya upimaji ambavyo vinapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa miongozo ya Baraza.

Kwa upande wa jamii, Baraza limetoa wito kwa wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano, kuhakikisha kuwa mitihani inafanyika kwa utulivu na kwamba maeneo ya shule yanaheshimiwa kama sehemu maalum ya upimaji.

Vilevile wananchi wote wamehimizwa kutoa taarifa kwa NECTA au mamlaka husika pindi wanapobaini vitendo vyovyote vya udanganyifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here