📌Wizara ya Nishati yasema elimu kwa maafisa dawati italeta mapinduzi ya kiafya na kimazingira
📌Mikoa ya Kanda ya Kati na Kaskazini wanufaika na elimu
📌Maafisa Dawati kutumia elimu hiyo kutekeleza azma ya Serikali
Na Mwandishi wetu, Singida
ELIMU ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia inayotolewa na Wizara ya Nishati kwa maafisa dawati na waratibu wa nishati safi ya kupikia katika halmashauri na mikoa yote nchini, inatarajiwa kuokoa vifo vya watu zaidi ya 33,000 kila mwaka vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia Wizara ya Nishati, Mhandisi Banezeth Kabunduguru wakati akiwasilisha mada katika mafunzo ya maafisa hao yaliyofanyika mkoani Singida tarehe 12 Novemba 2025.
Amefafanua kuwa, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 takribani watu 33,024 hufariki kila mwaka nchini Tanzania kutokana na athari za matumizi ya nishati isiyosafi ya kupikia.
“Zaidi ya watu milioni 3 duniani hufariki kutokana na athari za matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia ambapo asilimia 60 ya vifo hivi ni wanawake na watoto,”amesema Mhandisi Kabunduguru.

Amesisitiza kuwa kati ya vifo 500,000 hadi 700,000 hutokea Afrika na kwa Tanzania watu 33,024 hufariki kila mwaka hivyo elimu inayotolewa inalenga kuongeza kasi ya uelewa kwa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya Nishati Safi ya kupikia na hivyo kupunguza vifo hivyo.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa dawati, kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Yohana Dondi na Getrude Lamshai kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha wamesema kuwa elimu waliyoipata itawawezesha kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa ajenda ya nishati safi katika maeneo yao.
Wamesema kuwa, elimu hiyo itasaidia kuongeza taasisi na kaya zinazotumia nishati safi, kubadilisha mitazamo ya jamii, na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
“Kwa kuwa ajenda ya nishati safi ni mtambuka, tutaishirikisha jamii, taasisi, na wadau wote ili kuhakikisha tunapata matokeo chanya na kupunguza utegemezi wa nishati zisizo salama kama kuni na mkaa,” amesema Dondi.

Kupitia elimu hii, jamii inatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za kiafya, kimazingira, kijamii na kiuchumi zinazosababishwa na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
Pia, elimu hii itachochea maendeleo ya sekta ya nishati safi nchini na kusaidia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034.

Maafisa dawati na Waratibu kutoka halmashauri na mikoa ya Dodoma, Singida, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wameshiriki katika mafunzo ya siku moja ya Matumizi ya nishati safi ya kupikia mkoani Singida.



