Na Esther Mnyika, Dodoma
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu akitangaza Jina la Waziri Mkuu aliyeteuliwa na Rais baada ya kupokea ujumbe maalum kutoka kwa Mpambe wa Rais (ADC) Brigedia Jenerali Nyamburi Mashauri kuhusu uteuzi huo Bungeni leo Novemba 13, 2025.

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Dk. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jina la Mbunge huyo wa Iramba Magharibi limewasilishwa Bungeni kwa ajili ya Wabunge kumthibitisha kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemthibitisha Dk. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kura 369 baada ya kuteuliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Baadhi ya Wabunge wakitoa maoni kuhusu Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na Mbunge Mteule, Dk. Dorothy Gwajima amesema Dk. Nchemba ana utendaji kazi mkubwa na anapambania haki za watu hapendi kuona watu wana nyanyaswa.

“Anaamini katika jasho lako uweze kufanikiwa hivyo tunaamini atamsaidia sana Rais kuwaletea watanzania maendeleo zaidi,”amesema Dk. Gwajima.
Naye Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema amefanya kazi na Dk. Nchemba muda mtefu ni mchapakazi anayependa watu hivyo uteuzi wake unawaeleza watanzania kwamba mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi.

“Watanzania wategemee uongozi uliotukuka kwa sababu anakerwa na umaskini kutoka katika ya damu yake, siyo mtu anayefundishwa kuhusu maumivu ya umaskini, tumepata waziri mkuu bora katika historia ya nchi,”amesema.
Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Kigera amesema Dk. Samia amekidhi mioyo ya watanzania wengi na kuweka imani kwao kupitia uteuzi huo.
“Amekua ni mtu aliyefanya vizuri sana kwa kipindi cha miaka iliyopita akiwa Waziri wa Fedha miradi mkubwa mingi imefanyika, hasa kuongeza makusanyo,”amesema Mgore.
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Katavi, Martha Maliki amesema uteuzi wa Dk. Nchemba utaleta mapinduzi makubwa hususani katika sekta mbalimbali ikiwemo kusimamia utendaji wa wafanyakazi wa umma.


