Na Esther Mnyika, Dodoma
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amemtakia kheri Waziri Mkuu mpya wa Tanzania Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, akimtaka kuepuka vishawishi vya ndugu, jamaa na marafiki na badala yake ajielekeze zaidi katika kuwatumikia Watanzania.

Amebainisha hayo leo Ijumaa Novemba 14, 2025 Dk. katika hotuba yake muda mfupi baada ya kumuapisha Dk. Nchemba Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma, akimtaka kusimamia kikamilifu utekelezaji wa yale yaliyoahidiwa kwa watanzania wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu.

“Kwa umri wako mzigo huu ni mkubwa na vishawishi ni vingi kutoka kwa marafiki, ndugu, jamaa na wengine, nafasi yako hii haina rafiki, haina ndugu, haina jamaa- ni nafasi ya kulitumikia Taifa kwahiyo nikutakie kila la kheri katika utumishi wako,”amesema Dk.Samia.

Amesisitiza kuwa muda ni mchache katika kutekeleza yale waliyoahidi kwa wananchi, akimtaka kusimamia vyema baraza la Mawaziri kwa kutumia vyema uzoefu wake katika Wizara ya fedha na kumsimamia vyema atakayekuwa Waziri wa fedha ili fedha zipatikane katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Pia amempongeza Waziri Mkuu mpya wa Tanzania Dk. Mwigulu Nchemba kwa nafasi yake mpya ya utumishi, akisema jukumu lake la sasa ni kubwa na uteuzi wake umepitia ushindani mkubwa na katika vigezo kadhaa aliibuka mshindi kuliko wengine aliokuwa akishindana nao.

“Kubwa zaidi ni uwezo wa kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi zako na maelekezo yote yamo kwenye Katiba na nimekukabidhi vitabu vinavyoelekeza majukumu yako,” amesema.

Dk. Samia amemshukuru pia Majaliwa kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu, afya na mambo mengineyo, akisema amekuwa msaidizi mzuri katika kipindi chote alichofanya kazi kwenye serikali ya awamu ya sita.

Mara baada ya kumuapisha Dk. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa 14 wa Tanzania akichukua nafasi ya Kassim Majaliwa Majaliwa aliyeitumikia nafasi hiyo kwa takribani miaka kumi ikiwemo Mitano chini ya serikali ya Rais Dk.Samia.
Dk. Samia katika hatua nyingine leo mchana anatarajiwa kuzindua Bunge la 13 la Tanzania, akieleza kuwa katika hotuba yake ataeleza mwelekeo wa Serikali yake na vile vitakavyokuwa vipaumbele katika miaka mitano ijayo.


