Home KITAIFA Waziri Mkuu afanya ziara ya kushtukiza hospitali ya Mkoa wa Dodoma

Waziri Mkuu afanya ziara ya kushtukiza hospitali ya Mkoa wa Dodoma

▪️Atoa maagizo kwa Wizara ya Afya, MSD na hospitali zote nchini.

▪️Ataka wajawazito wasisubirishwe mapokezi wanapofika hospitali

▪️Wagojwa waipongeza Srtikali kwa kuboresha huduma za afya

Na Mwandishi wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba leo Novemba 15, 2025 amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuziagiza hospitali zote nchini zihakikishe wajawazito wanapofika hospitali wahudumiwe kwa haraka ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizaya ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na Hospitali zote nchini ziweke vipaumbele vya kuwa na dawa kulingana na mahitaji ya eneo husika.

“ Haipendezi mwananchi kufika hospitali na kupatiwa vipimo vyote kisha anaambiwa dawa akanunue kwingine, kama duka binafsi linaweza kupata dawa hizo, inawezekanaje hospitali za serikali hapati? Naagiza Hospitali zote ziwe na dawa,” amesema.

Ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi nje ya hospitali hiyo baada ya kutembelea wananchi waliofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali za kitabibu ambapo amesisitiza wananchi waendelee kuhudumiwa vizuri kwa kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma za afya nchini vikiwemo vifaa tiba na dawa.

Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zihakikishe zinakuwa na vifaa vya usafi binafsi vya dharura vikiwemo ndoo na beseni katika wodi za wazazi ili viwasaidie akinamama wasiokuwa na vifaa hivyo.

“Ujauzito sio suala la dharura vifaa kama ndoo tunapaswa kuwa navyo katika hospitali zetu za serikali.”

Dk. Mwigulu ametumia fursa hiyo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika uboreshaji wa huduma za afya nchini. Waziri Mkuu akiwa hospitalini hapo, wananchi walimueleza kuwa wanahudumiwa vizuri na kwa uangalizi wa karibu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza hospitali zote nchini zizingatie maelekezo ya kutumia mifumo sahihi ya malipo katika taratibu za kutoa huduma ili kuwezesha Serikali kuendelea kuhudumia wananchi.

Dk. Mwigulu ametoa agizo hilo kufuatia kuwepo kwa hospitali ambazo baadhi ya huduma wanapokea malipo kwa njia ya mtandao na nyingine malipo yanapokelewa malipo kwa njia zisizo rasmi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wagonjwa na wananchi wanaoguza ndugu zao wamempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma bora za afya.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tunapatiwa huduma nzuri kama tupo hospitali za private (binafsi).” Kauli hiyo imetolewa na Dinna Enock, mkazi wa Makulu jijini Dodoma ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here