Home KITAIFA Rais Dk. Samia: kachunguzeni uwepo wa taarifa kwamba vijana walilipwa fedha

Rais Dk. Samia: kachunguzeni uwepo wa taarifa kwamba vijana walilipwa fedha

Na Mwandishi wetu, Dodoma

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati wa Uchaguzi Mkuu kuchunguza taarifa za waandamanaji kulipwa fedha ili kuingia barabarani, na kujua fedha hizo zilitoka wapi.

Pia ametoa wito kwa Tume kuchunguza pia taarifa zinazodai kuwa baadhi ya vijana walilipwa fedha kabla ya kushiriki maandamano, na kubaini chanzo cha fedha hizo pamoja na mchango wa mashirika ya ndani na nje ya nchi katika tukio hilo.

Akizungumza Rais Dk. Samia wakati wa uzinduziTume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Alhamisi Novemba 20, 2025.

Amesema tukio la uvunjifu wa amani halikutarajiwa nchini kutokana na historia ya muda mrefu ya utulivu wa kisiasa na usalama ambayo Tanzania imeijenga tangu uhuru.

“Kwa hili lililotokea tumeona tuunde tume hii kwanza, ifanye kazi yake imalize. Mapendekezo yatakayotoka huku ndiyo tutakayoenda kuyafanyia kazi kwenye tume ile ya maridhiano. Kwahiyo, mapendekezo yenu ndiyo yatafanya ajenda kwenye Tume ya Maridhiano,”amesema.

Rais Dk.Samia amesema, Tume hiyo itafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu zilizoleta hali hiyo, ikiwemo kutathmini madai ya vijana walioingia barabarani kudai haki zao.

Aidha, amebainisha kuwa serikali inatarajia kujua ni aina gani ya haki ambayo vijana hao walihisi wameikosa.

“Tunatarajia Tume Huru ya Uchunguzi ituangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile. Tunataka kujua ni haki gani vijana walikosa na kwa nini waliamua kuingia barabarani kwa umoja wao kudai haki hiyo,” amesema.

Rais Dk.Samia amesema kuwa, wakati wa kampeni aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano ndani ya siku 100, lakini kutokana na matukio yaliyotokea, ameona ni muhimu kuanza na Tume ya Uchunguzi ili kupata taarifa sahihi zitakazowezesha hatua nyingine kufanyika kwa ufanisi.

“Wenzetu wanasema hawana imani na tume yoyote ya ndani, wanataka tume itoke UN, AU, Umoja wa Ulaya ndiyo zije zifanye kazi hapa kwetu Tanzania. Lakini mimi nina imani sana kwa ubobevu na uzoefu wenu, nina imani sana na tume hii.

Tume ya Uchunguzi ikimaliza kazi na kutuletea mapendekezo, ndipo tutajielekeza kwenye utekelezaji wake kupitia Tume ya Maridhiano kwa lengo la kuimarisha umoja na kuondoa changamoto za kisiasa,” amesema.

Kwa ujumla, hatua ya kuanzishwa kwa Tume hii inaonekana kuwa sehemu ya mwelekeo mpana wa Serikali katika kuendelea kuimarisha misingi ya uwazi na utawala bora.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here