Home KITAIFA Mpogolo atoa wito kwa viongozi kupambana na uwizi wa umeme

Mpogolo atoa wito kwa viongozi kupambana na uwizi wa umeme

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka viongozi wa serikali za mitaa, na madiwani, kuwa mstari wa mbele kupambana na wizi wa umeme katika maeneo yao.

Akizungumza leo Novemba, 20 jijini Dar es Salaam Mpogolo katika uzinduzi wa mafunzo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa Halmashauri za Manispaa za Ilala, Temeke na Kigamboni.

Amesisitiza umuhimu wa kuibua na kudhibiti watu wanaojihusisha na wizi wa umeme, akisema kuwa ni jukumu la viongozi hao kutoa taarifa na kushirikiana na taasisi husika kudhibiti uharibifu huu unaoharibu miundombinu ya umeme na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.

“Ndugu zangu viongozi, tuna jukumu la kuhakikisha kwamba tunakuwa macho katika maeneo yetu na kuibua matukio ya wizi wa umeme.

“Watu wanajenga, wanavunja majengo, lakini bado wanajiunganishia umeme kiholela. Hii ni hatari kubwa kwa usalama wa miundombinu yetu na pia inachangia kuleta vikwazo katika upatikanaji wa huduma bora za umeme,” amesema Mpogolo.

Ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wote walioweza kufika katika mafunzo hayo na kusema ushirikiano wao na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ni muhimu katika kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa usalama na kwa ufanisi katika maeneo yao.

Mpogolo ameongeza kuwa ushirikiano huu unahitajika kuepuka vikwazo vinavyotokana na uharibifu wa miundombinu ya umeme, hasa wakati wa shughuli za ujenzi.

Vilevile Mpogolo amegusia kuhusu majukumu ya viongozi katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za umeme, akisema kuwa wanapaswa kuwa daraja kati ya wananchi na TANESCO.

Amewahimiza viongozi wa mitaa na madiwani kuwa na ushirikiano wa karibu na TANESCO kuepuka migogoro na changamoto za umeme ambazo zimekuwa zikijitokeza katika baadhi ya maeneo, hasa mapya ya ujenzi kama vile Kariakoo na maeneo ya jiji.

“Ni muhimu kuwa na uwazi na ushirikiano katika kuhakikisha watu wanapata huduma za umeme kwa usalama. Viongozi wa mitaa na madiwani lazima wawe na jukumu la kuhakikisha watu wanapata huduma bora, lakini pia kuwaelimisha wananchi kuhusu hatari ya kujihusisha na wizi wa umeme,” amesisitiza Mpogolo.

Katika hatua nyingine, Mpogolo amewashukuru viongozi wa TANESCO kwa kubuni na kutoa mafunzo hayo kwa viongozi wa serikali za mitaa, akisema kuwa hatua hiyo ni ya muhimu kwa maendeleo ya huduma za umeme katika mkoa wa Dar es Salaam kwani lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtaa na kata inapata huduma za umeme kwa usalama, bila kuathiri miundombinu au kuleta changamoto kwa wananchi.

Mpogolo amesema serikali inawaunga mkono na itaendelea kutoa msaada kwa wale wanaohitaji msaada hivyo viongozi endeleeni kuhimiza ushirikiano kati ya serikali, TANESCO na wananchi kuhakikisha kuwa umeme unapatikana kwa usalama na bila vikwazo.

Pia amewahimiza viongozi wa mitaa na madiwani kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme, akisema kuwa kazi hiyo inahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, viongozi na TANESCO.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) K Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja TANESCO, Irene Gowelle amesema viongozi wa serikali za mitaa na madiwani aliowakutanisha ni kutoka wilaya za Ilala, Temeke na Kigamboni lengo ni kuimarisha mahusiano na kuhakikisha TANESCO inaboresha utoaji wa huduma za umeme kwa wananchi kupitia ushirikiano wa karibu na viongozi hawa.

Amesema TANESCO imeanzisha mkakati wa kuwasiliana na viongozi wa serikali za mitaa kwa madhumuni ya kujenga uhusiano imara na kuongeza ufanisi katika huduma kwa wateja.

Naye, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali ya Mitaa Dar es Salaam, Juma Abasi ameeleza kuridhishwa kwake na juhudi za TANESCO za kuboresha huduma za umeme nchini.

Amesisitiza kuwa shirika la TANESCO limefanya kazi nzuri kwa kushirikiana na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha uzalishaji wa umeme na kuhakikisha Tanzania inapata nishati ya kutosha kwa matumizi ya ndani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here