Home AFYA MOI na Ubalozi wa India na Jaipur kushirikiana kutoa miguu 600 bure...

MOI na Ubalozi wa India na Jaipur kushirikiana kutoa miguu 600 bure kwa watanzania

Na Amani Nsello- MOI

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Ubalozi wa India nchini Tanzania kupitia Taasisi ya Jaipur India inatarajia kuendesha kambi maalum ya kutoa miguu bandia kwa Watanzania 600 waliopoteza viungo hivyo.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Novemba 21, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Lemeri Mchome wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Dk. Lemeri amesema kuwa kambi hiyo itadumu kwa miezi miwili kuanzia Novemba 26, 2025 ambapo wahitaji watafika MOI kwa ajili ya usajili kabla ya kwenda eneo la Swami Vivekanand Cultural Centre (SVCC), Masaki Jijini Dar es Salaam

“Kambi hii ni ya miezi miwili, mhitaji atafika MOI kwa usajili… mpaka sasa wahitaji 300 wamejisajili, baada ya usajili Novemba 26, 2025 kambi hii itaanza rasmi eneo la Cultural Centre Masaki, Jijini Dar es Salaam,”amesema.

Dk. Lemeri ameongeza kuwa wahitaji watakaonufaika na huduma hiyo ni wale ambao wamepona kabisa majeraha ya kiungo alichopoteza na kwa wale ambao majeraha hayajapona wanashauriwa kusubiri wapone.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Siasa kutoka Ubalozi wa India nchini Tanzania, Lakshay Anand amesema kwamba wataalam watatumia teknolojia ya kipekee ya mguu wa bandia wa Jaipur Foot, ambapo mtu aliyekatwa mguu chini ya goti ataweza kutembea, kukimbia, kuchuchumaa, kupiga magoti, kucheza, kupanda mti, kuendesha gari na pikipiki.

Aidha Lakshay ametoa wito kwa wale wote waliopoteza viungo hususani miguu, wajitokeze kupata matibabu ya kambi hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here