Home KITAIFA Rais Dk.Mwinyi azindua mauzo ya nyumba za kisasa Kisakasaka

Rais Dk.Mwinyi azindua mauzo ya nyumba za kisasa Kisakasaka

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa nyumba za kisasa ili kuhakikisha kila mwananchi anapata makaazi bora kwa gharama nafuu.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba, 22 2025, wakati akizindua mauzo ya nyumba za miradi ya Kisakasaka B na Kisakasaka D, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakiuza viwanja bila kuzingatia uwepo wa huduma muhimu za kijamii kama maji, umeme na barabara, jambo ambalo limeathiri mpangilio mzuri wa miji. Kwa msingi huo, amesisitiza kuwa ni lazima kubuni mbinu mpya za upangaji ardhi mijini na vijijini.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi ameziagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kupiga marufuku uuzaji holela wa viwanja bila kufuata sheria na matumizi bora ya ardhi.

“Natamani kuona mabadiliko makubwa katika sura ya miji na vijiji, akiwataka wananchi kuachana na mtazamo wa kuishi katika nyumba chakavu, akitaja maeneo ya Michenzani na Kikwajuni kama mifano ya makaazi yaliyopitwa na wakati,”amesema.

Ameongeza kuwa katika awamu ya pili ya Serikali ya Awamu ya Nane, Serikali imejipanga kuboresha maeneo mbalimbali ikiwemo Jang’ombe, Kwahani na Kilimani, ili kuacha alama kupitia ujenzi wa nyumba bora za kisasa.

Akizungumzia mradi wa Kisakasaka, Dk. Mwinyi amesema eneo hilo litakuwa mji wa kisasa wenye huduma kamili kama maji, umeme na barabara, na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa ya kununua nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC).

Wakati huo huo, amewashauri watumishi wa umma kuchukua mikopo ya nyumba badala ya kukopa vifaa vya ujenzi, ambavyo huchelewesha ukamilishaji wa nyumba na kuathiri hali za kiuchumi. Amesema Serikali itawawezesha watumishi kupitia nyongeza ya mishahara na mpango wa mikopo yenye makato madogo kwa kipindi cha hadi miaka 25.

Rais Dk.Mwinyi amekemea tabia ya kuwapa miradi wakandarasi waliowahi kushindwa kutekeleza kazi kwa wakati, akiahidi hatua kali kwa watendaji watakaokiuka maagizo hayo.

Vilevile, amezitaka Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuacha kujenga nyumba za watumishi na badala yake kununua nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba ili kupunguza gharama.

Ameielekeza ZHC kuhifadhi asilimia 40 ya nyumba zote kwa ajili ya wananchi wenye kipato cha chini ili nao waweze kukodishwa nyumba hizo.

Rais Dk. Mwinyi amelipongeza Shirika la Nyumba kwa kazi nzuri wanayoifanya, akilitaja kuwa miongoni mwa mashirika bora nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here