Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
UPANDE wa mashitaka katika kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara watatu wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa jengo la Kariakoo, umedai kuwa utakuwa na mashahidi 55 na vielelezo 54 wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni mkazi wa Mbezi Beach na mfanyabiashara, Leondela Mdete (49), mkazi wa Kariakoo, Mwarabu Zenabu Islam (61) na mfanyabiashara na mkazi wa Ilala, Ashour Awadh Ashour (38). Wengine ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Beach, Sosteri Nziku (55), mfanyabiashara Aloyce Sangawe (59) na mfanyabiashara Stephen Nziku (28).
Hayo yalisemwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Geofrey Mhini kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusomwa kwa hoja za awali. “Upelelezi wa kesi umekamilika na tayari tumekwishapeleka taarifa Mahakama Kuu na hapa tunasubiri mwongozo wa mahakama yako ili tuweze kuendelea,” alisema.
Hakimu Mhini amesema ni kweli taarifa zimekwishatumwa kwake kutoka Mahakama Kuu na anatarajia kesi hiyo isomwe siku mbili mfululizo. “Kesi hii ina vielelezo 54 na mashahidi 55, kwa muda tulionao sasa hatuwezi kumaliza, hivyo naona tusome hoja za awali siku mbili mfululizo ili tumalize tuweze kuanza usikilizaji,” alisema Mhini.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 3 na 4 mwaka huu. Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ilidaiwa Novemba 16, 2024, maeneo ya Mchikichi na Kongo, Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, isivyo halali washitakiwa kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31.
Marehemu hao ni Said Juma, Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu, Rashid Yusuph na wengine. SOMA: Waliofia Kariakoo kuagwa mchana huu



