Home KITAIFA Ulega aagiza tathmini barabara ya nje ya jiji la Arusha

Ulega aagiza tathmini barabara ya nje ya jiji la Arusha

📌 Itakuwa suluhisho la msongamano wa magari katikati ya jiji
📌Atoa rai wananchi walinde miundombinu.

Na Mwandishi wetu, Arusha

WAZIRI Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Arusha kufanya tathmini na kuwasilisha mpango kazi katika ofisi yake kuhusu barabara ya mzunguko ya Tengeru – Mirerani yenye urefu wa kilometa 28 ili kusaidia kupunguza msongamano wa malori katikati ya jiji la Arusha.

Ulega ametoa maelekezo hayo mkoani Arusha wakati akikagua maendeleo ya ujenzi mradi wa dharura wa makalvati matatu na uinuaji wa tuta lap barabara katika eneo la King’ori barabara kuu ya KIA JCT – Namanga.

Waziri Ulega ameeleza utekelezaji wa mpango kazi huo utashirikisha Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Usalama Barabarani kuelekeza malori yatumie barabara hiyo ili barabara kuu iendelee kutumika kwa shughuli za kuinua utalii.

Aidha, Ulega ametoa wito kwa watanzania kuilinda miundombinu ya barabara, taa na samani za barabara zinazowekwa kwani inagharimu fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kutekelezwa katika miradi mingine.

Naye, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema kutokana na uboreshwaji wa Bandari ya Tanga idadi ya malori yanayopita katika barabara ya KIA – Arusha imeongezeka hivyo inasababisha msongamano wa malori na magari ya watalii katikati ya jiji la Arusha na hivyo kumuomba Waziri Ulega kutatua kero hiyo kwa kupata barabara ya mzunguko itakayotumiwa na malori.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Massawe amesema mradi huo wa makalvati makubwa matatu unatekelezwa na Mkandarasi M/s Abemulo Contractors na kusimamiwa na Kitengo cha TECU – TANROADS kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.6 ambapo mpaka sasa utekelezaji wake umefikia 94 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2025.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here