Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan amesema matukio ya Uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 yalikuwa matukio ya kutengeneza yakidhamiria kuangusha Dola ya Tanzania.

Hayo ameyaeleza leo Disemba 2, 2025 Dk.Samia wakati akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar Es Salaam kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, amesema Vijana wa Kitanzania walifanywa makasuku na kuimbishwa.
“Vijana wetu walifanywa makasuku na kuimbishwa kabisa yaliyotokea Madagascar yatokee na hapa. Lakini ukimvuta kijana pembeni ebu niambie Madagascar kumetokea nini hajui, unataka hapa kitokee nini? Hajui lakini waliimbishwa wimbo huo,” amesema.
Ameeleza kuwa vurugu zile ni mradi mpana wenye nia pana ya uovu ulio na wafadhili na watekelezaji, akisema katika vurugu ile wengine waliingia bila ya kujua na kufuata mikumbo huku wengine pia wakijihusisha na vurugu zile kwa hadaa za maisha mazuri, huku wengine wakilipwa fedha ili kushiriki katika vurugu zile.
Akionesha kuumizwa na madhara yaliyojitokeza wakati wa matukio hayo ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025, Dk.Samia ametaka mjadala wa pamoha, akihoji ikiwa yale yalikuwa maandamano ama vurugu na uharibifu wa mali za umma.

Ameongeza kuwa kilichotokea Oktoba 29, 2025 hakikuwa maandamano bali ni vurugu zilizoandaliwa kwa madhumuni maalum hivyo nguvu iliyotumika kuyadhibiti inaendana na tukio husika.
“Takwimu zinatolewa sasa hivi, kuna majengo kadhaa ya Serikali yameunguzwa, kuna miradi kadhaa iliyojengwa kwa maslahi ya Wananchi imeunguzwa, Vituo vya mafuta, biashara binafsi za Watu, magari ya Serikali, vituo vya Polisi vingi tu vimeunguzwa, sasa nataka tuwe na jina la hayo ni maandamano au vurugu? maandamano tuliyoyazoea na kuyakubali ndani ya Katiba ni yale Watu wameudhika na kitu tunaomba tuandamane tueleze tutatoka point moja hadi Mnazimmoja au popote pengine na mabango yanaeleza maudhi yetu na Polisi wanawasindikiza vizuri hadi wanapofika”
“Haya ya kuunguza miradi ya Serikali, vituo vya Polisi na kwenye kituo cha Polisi unakwenda kufanya nini? ni kwenda kuvamia na wapate silaha, madhumuni ya kuwa na silaha mkononi ni nini? haya hayakuwa maandamano zilikuwa vurugu zilizoandaliwa kwa madhumuni maalum”
“Serikali inawajibu tunaapa kuilinda mipaka ya Nchi hii na kulinda Raia na mali zao, katika hali hiyo nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo, sasa tunapoambiwa tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile… nguvu ndogo ilikuwa ni ipi?, ilikuwa tuwangalie Waandamanaji waliojiandaa kufanya mapinduzi mpaka wafanikiwe? hapo patakuwa pana Dola kweli? Dola haipo hivyo”
“Na sio Tanzania tu hata Mataifa mengine Watu wakiandamana wanaweka nguvu kubwa, sasa wanapokuja kutulamu mlitumia nguvu kubwa wao walitaka nini?, tujiulize je hawa ndio Wafadhali wa kile kilichofanyika? walitaka tuangalie ile mob hadi ifanikiwe walichowapa fedha, walichowatuma? hapana” tuliapa kulinda Nchi hii na mipaka yake , usalama wa Raia na mali zao kwahiyo kama wanavyofanya wao na sisi tutafanya vilevile kuilindi Nchi yetu,” amesema.
Dk. Samia amesema Vijana wengi wa Tanzania hawana uzalendo na hilo Serikali imejifunza na italifanyia kazi huku akisisitiza kuwa Vijana hawajaandamana sababu ya ugumu wa maisha bali ni kwakuwa walilipwa na wengine walifuata mkumbo.

“Vijana wetu wameingizwa barabarani wakaimbishwa wimbo wasioujua wanadai haki, haki gani!?, mvute Kijana pembeni muulize unadai haki gani!?, na hiyo haki hawakuweza kuidai kwa njia gani hadi waingie njiani wafanye vurugu?, walipwe wakachome vituo?, jingine wanalobebeshwa wameingia njiani eti kwa ugumu wa maisha, Astaghfrullah, ningekuwa na uwezo ningewabeba Vijana wa Tanzania nikawatupe kwenye nchi kadhaa za Afrika pamoja na Majirani zetu wakaone ugumu wa maisha uliokuwepo, halafu waseme kwamba kwao Tanzania ni pahala pema.
Mwenye ugumu wa maisha kwa raha zake kabisa kweli ataingia njiani akaimbe woyoo woyoo huo ugumu wa maisha?, wenye ugumu wa maisha ataingia kupambana kutafuta chakula, hawa hawakuwa na ugumu wa maisha walikuwa na sababu zao nyingine, Watafiti wafanye utafiti waangalie nafasi ya Tanzania kwenye ugumu wa maisha,” ameeleza.
“Vijana wetu wasimezeshwe tu na wenyewe wakameza hapana, haya yanatokea tumejifunza kwamba Vijana wetu wanakuwa tu bila elimu ya uzalendo, Vijana Wazalendo hata upinzani hawakukubaliani na lile, walikuja kutuambia kaeni vizuri wanapanga kufanya hivi, Vijana wetu wengi Tanzania sio Wazalendo na hilo Serikali tumejifunza na tutakwenda kulifanyia kazi.
Na ndio maana nimeunda Wizara nzima ya Vijana ili kushughulikia Vijana kwa uapana, kwahiyo Vijana wetu hawakuwa na sababu ya msingi ya kuingia barabarani isipokuwa kutumwa na kuingilia mambo yasiyowahusu,”amesema.
Pia ametoa pole kwa wale wote walioondokewa na Ndugu, Jamaa na Watoto wao wakati wa maandamano ya October 29,2025 na waliouawa baada ya maandamano ambapo amesema Mtanzania mmoja akiondoka ni msiba wa Watanzania wote.
“Inatia uchungu kuona wachache walioratibu fujo zile wakitaka Watanzania wenzao wawe kafara kwa malengo yao ya kisiasa yaliyojaa ubinafsi, malengo yao ni tofauti na siasa zilizopo lakini kwasababu zozote zile hatukupaswa kuvuruga amani ya nchi yetu wala kusababisha vifo kwa watu wetu.
Kwa wale walioondekewa na Ndugu zao, na Watoto wao na Jamaa zao natoa tena pole kwa sote sio msiba wao pekee yao ni wetu wote kwani damu ya Watanzania ni damu yetu sote, Mtanzania mmoja akiumia tumeumia wote, kuondokewa na Mtanzania mmoja tumeondokewa wote,”amesema.

Dk. Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni huru na haitoingiliwa na serikali ama chombo kingine chochote kutoka nje ya Tanzania, akisema fedha chache wanazozitoa kwa Tanzania si kigezo cha kuingilia mambo ya Tanzania.
Amesema Tanzania imeumbwa vizuri na kuwekwa pazuri katika soko na siasa za dunia na ndilo tatizo linalosababisha kupigwa vita.
“Nje huko wanakaa kuwa Tanzania ifanye hili na hili halafu ndiyo itakuwa hivi, who are you? Niwaulize ndugu zangu, kwao hayatokei? Tumenyanyua sauti sisi kusema ya kwao? Wanadhania kuwa bado wao ni master wetu, ni wakoloni kwetu? Kitu gani? Ni fedha chache wanayotugaia? Na fedha yenyewe sasa hivi haipo, tunafanya biashara wao wapate na sisi tupate,” amesisitiza.
Amesema Tanzania kutofungamana na upande wowote pamoja na uwepo wa rasilimali nyingi ikiwemo bahari, madini na Maziwa kumeifanya Tanzania kuwa muhimu kiuchumi duniani suala ambalo limewanyima usingizi Mataifa mengi duniani.
Rais Samia amewaambia watanzania kuwa maumbile na Utajiri wa Tanzania ni muhimu kila mmoja kutoruhusu kuwa laana na sababu ya Watanzania kuuana kwa kushawishiwa na wanaoitolea macho Tanzania, akisisitiza kuwa huu ni wakati muhimu wa kushikamana na kuendeleza umoja wa Watanzania.
TUMEJIPANGA NA WANAOJIPANGA NA DISEMBA 9_25
Rais Dk.Samia akizungumzia kuhusu Disemba 9- 25 amesema serikali na Vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga wakati wote kukabiliana na wanaoratibu, kupanga na kufadhili matukio ya uvunjifu wa amani yaliyopangwa kufanyika aidha Disemba 09 ama Disemba 25, 2025.
Amsema kwamba matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 yalikuwa ni matukio ya kupangwa yakiwa na lengo la kuiangusha dola ya Tanzania.
“Ndugu zangu nilisema yaliyopita si ndwele tugange yajayo, lililopita limepita, kwa maneno tunasikia lipo jingine linapangwa lakini inshaallag Mola hatosimama nao, litapeperuka.
Lakini nataka niseme, nilimsikia mmoja kati ya waandaaji wa nje anasema ebu tarehe tisa lihairisheni subirini Krismasi kwasababu sasa hivi wamejipanga, nataka niwaambie wakati wowote wakija tumejipanga,”amesema.
Aidha amesema kama binadamu kukosana kupo, akikiri kuwa si kila wakati serikali inakuwa haina mapungufu, akisisitiza umuhimu wa kukaa, kuzungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo nchini kama njia sahihi ya kuondoa tofauti na migogoro iliyopo



