Home UCHUMI Serikali inatambua mchango wa TCB kupanua wigo wa huduma jumuishi za...

Serikali inatambua mchango wa TCB kupanua wigo wa huduma jumuishi za fedha

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

SERIKALI, imesema inatambua na kuthamini mchango wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha kwa wanawake na wajasirimali wadogo na wa kati .

Hayo yamebainishwa leo Disemba, 3 2025 Jijini Dar es salaam jana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ,Elijah Mwandumbya wakati akimwakilisha Waziri wa fedha Balozi Khamis Mussa Omar katika Hafla ya kutangaza matokeo kuorodheshwa kwa dhamana ya Ustawi Bond iliyopo chini ya Benki ya Biashara Tanzania (TCB)

Amesema TCB ni benki ya kibiashara, yenye historia, tamaduni na urithi uliojaa utajiri wa miaka zaidi ya 100 katika kuhudumia Watanzania kutoka katika kila sehemu ya nchi .

“Utoaji wa Ustawi ya hatifugani ya Ustawi Bond ni uthibitisho wa dhamira ya Benki hiyo kuunga mkono Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 pamoja na Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21-2029/30 ambao unalenga upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kupitia masoko ya mitaji na dhamana katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi,”amesema.

Amesema kuwa Kupitia ukusanyaji wa mtaji wa muda mrefu kupitia Stawi Bond, utaongeza uwezo wake wa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali wadogo na wa kati wakiwemo wanawake na vijana.

“Hatua hii itawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuboresha ustawi wa jamii na ajira hivyo nawapongeza kwa kupata idhini rasmi ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kuhusu utoaji wa Stawi Bond, hatua iliyowapa wawekezaji uhakika muhimu wa kuwekeza kwenye dhamana hii”amesema

Aidha ameipongeza Benki ya TCB kwa mafanikio makubwa waliyoyapata katika utoaji wa hatifungani ya Stawi Bond, ubunifu ambao ni wa kipekee na wenye mwelekeo mpya wa kuongeza mtaji wa benki na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo, alisema kuwa matokeo hayo ni hatua muhimu ya kihistoria kwa benki na kwa masoko ya mitaji nchini kwa ujumla.

“Ukusanyaji wa Shilingi bilioni 140.24, karibu mara tatu ya lengo letu la awali unaonesha imani kubwa ambayo Watanzania wameiweka katika dira ya TCB pamoja na dhamira yetu ya kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi,” amesema Mihayo

“Kinachofanya hatua hii kuwa ya kipekee zaidi ni ushiriki mkubwa na wa kiwango cha juu kutoka kwa wawekezaji wadogo na wa kati yaani Watanzania wa kawaida waliotumia fursa hii kuwekeza katika bidhaa salama na yenye tija,”amesema.

Amesema tofauti na hatifungani nyingine ambazo mara nyingi hutawaliwa na uwekezaji wakubwa wa mashirika na kampuni, Hatifungani ya Stawi ilivutia ushiriki mkubwa kutoka kwa wawekezaji binafsi.

“Hii ni ishara muhimu ya kuimarika kwa ujumuishi wa kifedha na ongezeko la ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji,”amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CMSA, Nicodemus Mkama, amesema mafanikio ya deni hilo yanaonesha ukuaji endelevu na mabadiliko katika masoko ya mitaji nchini.

“Hatua hii inawezesha benki kuongeza ukwasi na kuimarisha mtaji wake, jambo litakaloiwezesha TCB kuboresha zaidi ufanisi wa huduma zake na kuwafikia wajasiriamali na wananchi kwa upana,” amesema Mkama.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inatoa msingi imara na kufungua milango kwa taasisi nyingine za serikali na sekta binafsi ambazo zimeonesha nia ya kutumia masoko ya mitaji kutafuta fedha kwa ajili ya biashara na miradi ya maendeleo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here