Home KITAIFA Tanzania yashinda Tuzo ya dunia katika sekta ya utalii

Tanzania yashinda Tuzo ya dunia katika sekta ya utalii

Na Esther Mnyika, Dar es Salaam

TANZANIA imepata tena heshima kubwa baada ya kushinda tuzo ya dunia katika sekta ya utalii wa safari kwa mwaka wa pili mfululizo, ikitambuliwa kama nchi bora zaidi duniani kwa utalii wa safari.

Tuzo hiyo ni kubwa zaidi katika sekta ya utalii na ni ushindi wa kihistoria na matokeo ya juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuhifadhi na kukuza utalii.

Akizungumza leo Disemba, 8 2020 jijini Dar es Salaam wakati akiwasili na tuzo hiyo nichini Katibu Mkuu Wizara Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza utalii huku akiitaja filamu maarufu ya Royal Tour na Amazing Tanzania kama sehemu ya jitihada za kutangaza vivutio vya nchini.

Amesisitiza kuwa tuzo hii ni matokeo ya uhifadhi bora wa wanyama na mazingira, jambo ambalo limetangaza Tanzania kama kivutio kikubwa kwa watalii duniani.

Dk. Abasi ameeleza kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa tuzo hizo za dunia mwakani na mashirika yote makubwa ya utalii na wadau wa sekta hiyo watawasili nchini.

“Sasa dunia inakuja Tanzania, badala ya Tanzania kufuata tuzo hizi. Hii ni fursa kubwa kwa nchi yetu kuwa kivutio cha kimataifa, si tu kwa utalii wa safari bali pia kwa shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii,”amesema.

Aidha, Dk. Abasi ameeleza kuwa sekta ya utalii imeendelea kukua kwa kasi tangu kumalizika kwa janga la COVID-19, ambapo idadi ya watalii iliongezeka kutoka 600,000 hadi kufikia milioni 2.1 mwaka jana.

Amesema hali hiyo imechangiwa na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na sekta binafsi, ambao wamejizatiti katika kukuza na kutangaza vivutio vya Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Nchini(TTB), Ephraim Mafuru ameshukuru wadau wa sekta ya utalii kwa michango yao katika kuhakikisha Tanzania inashinda tuzo hiyo.

Amesisitiza kwamba ushindi huo unathibitisha dunia imetambua ubora wa vivutio vya utalii vya Tanzania, hasa Hifadhi ya Serengeti ambayo ilishinda tuzo ya Hifadhi Bora Duniani.

Mafuru ameongeza kuwa Tanzania imekuwa na mafanikio makubwa katika uhifadhi kwa sababu sio tu nchi yenye vivutio vya wanyapori bali maeneo mengi ya kipekee.

“Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha miundombinu ya utalii, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara katika maeneo ya hifadhi, huku tukiwa na vivutio vingi vya kipekee, ikiwemo mapori ya akiba na misitu jambo linaloifanya kuwa nchi bora kwa utalii wa safari duniani,”amesema.

Mafuru amewaambia Watanzania kuwa tuzo hizo ni ishara ya mafanikio makubwa na ni muhimu kwa kila mtu kushiriki katika juhudi za kuendeleza utalii na uhifadhi.

Amesisitiza kuwa utalii ni sekta inayochangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa hivyo Tanzania imejipanga kuwa kivutio kikubwa zaidi duniani kwa utalii wa safari na vivutio vyake vya asili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here