Na Esther Mnyika,Dar es Salaam
KITUO cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (MECIRA) kimehimiza jumuiya za ndani kuendelea kulinda amani mshikamano wa kitaifa maelewano ya kidini kuepuka kuruhusu kutumiwa au kushawishiwa kujiingiza katika mipango ya vurugu au machafuko.

Pia Jumuiya za Kimataifa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kisheria katika kudhibiti uhamasishaji wa vurugu unaofanyika kupitia mipaka ya nchi, kikisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu kulinda amani na mshikamano wa Tanzania.
Akizungumza leo Disemba 17,2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa MECIRA, Habibu Mchange, amesema kituo hicho tayari kimeziarifu Serikali za Marekani na Kenya kuhusu uwepo wa watu wanaotumia nchi hizo kama majukwaa ya kusambaza taarifa potofu na kuchochea machafuko dhidi ya Tanzania.
“Vyombo vya Habari wanaharakati na viongozi wa kijamii kutumia uhuru wao kwa kuwajibika, wakitambua kuwa maneno na ujumbe vinaweza kusababisha madhara makubwa na vijana kutambua kuwa kushiriki katika uhamasishaji wa machafuko kunaweza kusababibashia madhara ya kisheria, kijamii na kifamilia,”amesema.
Mchange amesema kuwa ingawa Tanzania inatambua na kuheshimu misingi ya demokrasia, haki za binadamu na uhuru wa kujieleza, misingi hiyo haiwezi kutumika kama kisingizio cha kuhalalisha vitendo vinavyohatarisha maisha ya watu au kuvuruga amani ya taifa jingine.
Amesisitiza kuwa uhuru wa kujieleza una mipaka ya kisheria na lazima uendane na uwajibikaji, hasa pale unapovuka mipaka ya maoni na kuingia katika uhamasishaji wa vurugu, chuki au machafuko ya kijamii na kisiasa.
Ameeleza kuwa hakuna raia anayepaswa kutumia nchi ya kigeni kama kimbilio au jukwaa la kupanga, kuratibu au kuhamasisha vitendo vya vurugu dhidi ya nchi yake, akiongeza kuwa hatua kama hizo zinakiuka misingi ya sheria za kitaifa na kimataifa.
Ameongeza kuwa wahusika wote waliodaiwa kuhusika katika uhamasishaji wa machafuko yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali Oktoba 29, 2025, wanapaswa kuwajibishwa kisheria bila kujali wanapoishi au walipojificha.
Mchange ameeleza kuwa kanuni ya uwajibikaji binafsi wa jinai imethibitishwa kimataifa, hususan katika kesi za wahamasishaji wa machafuko makubwa na mauaji ya kimbari, ambapo wahusika wamechukuliwa hatua za kisheria hata wakiwa nje ya nchi walikotenda uhalifu.
Aidha, ametoa wito kwa Serikali ya Marekani kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kisheria, ikiwemo kuwezesha kurejeshwa kwa baadhi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na uhamasishaji wa vurugu ili wakabiliane na sheria kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu taarifa kwamba baadhi ya watanzania wanaoishi au kukimbilia nchini Kenya wanadaiwa kuendelea kupanga na kusambaza ujumbe unaohatarisha amani ya Tanzania kupitia mitandao ya kijamii.



