Na Esther Mnyika, Dar es Salaam
WAZIRI wa Maendeleo ya jamii ,jinsia wanawake na makundi maalum Dk. Doroth Gwajima amesema kuwa watoto wengi wanaofikia hatua ya kujinyonga hukosa watu wa karibu wa kuzungumza nao ili kueleza hasira, maumivu na changamoto wanazopitia.

Pia amesema Serikali inaendelea kutekeleza ajenda ya taifa ya kuwekeza katika afya na maendeleo ya vijana balehe nchini kwa mwaka 2021 /2022 hadi 2024/2025 ambapo ajenda hiyo inahamasisha umuhimu wa huduma bora za afya na maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.mgeni
Hayo ameyasema leo Disemba, 22 2025 jijini Dar es Salaam Dk. Gwajima wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo na fursa mbalimbali kwa makundi maalum kwa mwaka 2025/2026.
“Matukio ya watoto kujinyonga kwanza tuanze kujua dalila za mtoto anaelekea kuchukua maamuzi magumu haraka kabla hajachukua maamuzi hayo haya ni masuala ya malezi,” amesema
Ameongeza kuwa mawasiliano ndani ya jamii zetu yako je? Na watoto wetu wanaamka saa kumi usiku kwenda kwenye kibarua wanarudi saa sita usiku watoto wamelalq wanakutwa na madhira gani na nani anazungumza nao.
Amesema wazazi wanatenga siku ngapi? Kwa mwezi au wiki kungumza na watoto kujua yanayo wasibu hivyo watoto wanapata hasira hawana mtu wa kumwambia.
” Niliona mtoto kajinyonga kakosa gauni la Krismasi tukio lilikotokea watu wote wanaelewa uwezo wa mzazi hivyo wanaburudika wazazi tunawajenga je? Kwenye saiklojia maisha yetu ni haya tufanya hivi,” amesema.
Pia ameomba wazazi kuwekeza kwenye makuzi na malezi bora ambapo akikerwa atakuambia na akikosea unamwambia bondi nzuri kati ya mzazi na mtoto
Amesema katika kuimarisha wajibu wa wazazi katika Malezi ya vijana balehe, Serikali inatekeleza Programu ya Malezi ya Vijana Balehe inayojulikana kama Furaha Teen inayotekelezwa kwa majaribio katika Mikoa ya Songwe na Mbeya.
Aidha amesema Kupitia programu hiyo wazazi wanafundishwa mbinu za kuwalea na kuwaongoza watoto wao ili waweze kukabiliana na changamoto za ujana balehe.
“Natoa wito kwa wazazi kuhusu umuhimu wa kuwasikiliza na kuwashirikisha vijana wao katika shughuli mbalimbali za kifamilia na kijamii sambamba na kuwaongoza kwenye masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ili kuwaepusha na tabia na mwenendo isiyofaa katika jamii,”amesema.
Amesema katika kujenga jamii yenye usawa na yenye haki, ni muhimu pia kuzingatia usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha hivyo kwa kutambua hilo, Serikali imeweka mazingira rafiki na wezeshi kwa makundi maalum hususani wanawake kushiriki kufanya maamuzi katika ngazi mbalimbali za uongozi, kuendelea kuweka mifumo ya kukuza vipaji kwa wasichana na wanawake na kutoa mafunzo endelevu ya uongozi na utawala bora.
Amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi, program na kampeni mbali mbali katika jamii zinazohusu huduma za malezi , hifadhi ya jamii,unasihi, Afya ya akili, Msaada wa kisaikolojia na kijamii,elimu, lishe,matunzo ya watoto,marekebisho ya tabia,utengamao,ulinzi watoto na wazee, huduma za uangalizi wa wafungwa na mahabusu,usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia,kuunganisha wahudumiwa katika familia na jamii, na kuwaungunisha wahitaji na watoa huduma mtambuka.
Ameeleza kuwa utoaji wa huduma ya ulinzi na matunzo kwa Wazee na Wasiojiweza imeendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa unaohusisha Serikali na Watoa Huduma binafsi ambapo katika kipindi cha 2022 hadi 2025, Wizara imetoa huduma za msingi za chakula, malazi, mavazi na matibabu utoaji bima ya afya bila malipo ambapo jumla ya Wazee 1,256,544 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bila malipo pamoja bima za afya.
Aidha, serikali inaendelea kutoa huduma za matunzo kwa wazee katika Makazi ya Wazee 13 yanayomilikiwa na Serikali ambayo ni Makazi ya Wazee Kibirizi (Kigoma), Njoro (Kilimanjaro), Kolandoto (Shinyanga), Bukumbi (Mwanza), Ipuli (Tabora), Fungafunga (Morogoro), Mwanzange, Misufini (Tanga), Nunge (Dar es salaam), Nyabange (Mara), Kilima (Kagera), Sukamahela (Singida) na Magugu (Manyara) yenye jumla ya Wazee 245 (Me 147, Ke 98).



