Home KITAIFA Ni muhimu hoja za vijana kusikilizwa na kupatia ufumbuzi-Askofu Kisare

Ni muhimu hoja za vijana kusikilizwa na kupatia ufumbuzi-Askofu Kisare

Na Mwandishi Wetu, Mara

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania Nelson Kisare, amesema ni muhimu hoja za vijana kusikilizwa na kupatiwa ufumbuzi na sio kutumia nguvu kuwadhibiti kwani kufanya, hivyo ni kutengeza bomu ambalo litalipuka na kuleta madhara.

Kisare ameyasema hayo hivi karibuni mkoani Mara kwenye Warsha ya Viongozi wa Dini iliyoandaliwa na Kanisa hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), na kubeba kauli mbiu inayosema “Elimu ya Amani, Taifa Salama.

Amesema amani lazima iwe moyoni, watu wawe na matumaini ya maisha yao ya kesho, keshokutwa na mbele ya safari, mtu aone matumaini mbele yake na wasikate tamaa.

Askofu Kisare amesema ni muhimu vijana kusikilizwa kwamba kuna nini huko kwao na wanataka nini na sio kuwapuuza.

“Sisi viongozi wa dini, kijamii na serikali hatujawapa vijana nafasi ya kusema na kuwasikiliza wanataka nini, tunatumia nguvu nyingi sana ya kuwanyamazisha haitatusaidia, ni lazima tuwasikilize, wana mambo yao yanayowaumiza katika mioyo yao.

Hata kama tunatofautiani, kutofautiana sio jambo baya, kutofautiana kunaleta maendeleo, hebu fikiria kama dunia yote ingekuwa haitofautiani je maendeleo yangepatikana. Kama mawazo yote yangekuwa sawa, hivyo kama wewe ni mwizi watu wote wakufuate,” amesema.

Amesema kilichotokea ni matokeo ya vijana kutosikilizwa na jamii yao, hivyo baada ya kutosikilizwa waliamua waende kwa baba yao ambaye anaitwa mitandao ya kijamii, ambaye amewasikiliza na kupanga mipango na matokeo yake ndio yameanza kutokea.

“Sisi viongozi wa dini, siasa na kiserikali tunawatumiaji hao vijana, wengine wanawatumia kutekeleza mapenzi na matakwa yao ovu, kwa kuwa wanatambua hawana ajira wala fedha. Ni wajibu wetu kama viongozi wa dini kuendelea kuwalea vijana wetu katika maadili mema kwa kumcha Mungu na kuwasaidia nini wafanye,” ameongeza.

Amesema jambo kubwa ambalo linahitajika ni vijana kusikiliza na wasizuiwe kusema kwani kufanya hivyo kunatengeneza bomu siku za mbele na bomu hilo likilipuka hakuna atakayeweza kuzuia kwani wapo wengi.

Askofu Kisare amesema vijana hao wana mawazo mazuri, lakini hawashirikishwi kuyatoa, jambo ambalo halina afya kwa maslahi ya nchi.

Amesema Mungu hapendi ukimya unaolinda uovu, bali watu wake wanapaswa kusimama upande wa haki, kweli na utu wa binadamu.

“Ukisoma Kitabu cha Mika Sura sita, mstari wa nane, unasema ee mwanadamu yeye amekuonyesa yaliyo mema na bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki na kupenda rehema na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako,” amesema.

Askofu huyo amesema Mungu anatamani watu wanaotenda haki, wanaopenda rehema, wanaopenda kutenda haki kwa watu wengine, matendo yaliyomema, yakufariji, matumaini na kuwapa nguvu ya kuamini kuna kesho yake.

Aidha, Askofu Kisare amesema kuna changamoto nyingine ya viongozi wa siasa kutumia lugha za matusi, chuki na kejeli kwani kufanya hivyo wanamuuzi Mungu.

Ametoa rai kwa viongozi kuacha tabia ya upendeleo katika kutimiza majukumu yao, kwani hali hiyo inajenga chuki kwa jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema mkutano huo umeandaliwa ili kutoa fursa kwa wadau kujadiliana kuhusu amani ya nchi yao.

Amesema wameamua kuchukua jukumu hilo la kutoa elimu ya uzalendo ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuelekea kwenye maridhiano ya kitaifa.

“Tunabebwa na itikadi ya uzalendo, hivyo tunaamini kupitia mikutano hii, tutaeweza kumsaidia Rais katika kujenga Taifa bora,” amesema.

Naye Dk Musuto Chirangi, amesema kilichotokea hivi karibuni kinatokana na matabaka ambayo yameibuka kwenye jamii, hivyo ni muhimu kuangalia upya eneo hilo.

“Tumeshuhudia matabaka ya walio soma na wasio soma, wenye nacho na wasio nacho, dini kwa dini, hivyo katika mazingira hayo ni lazima jamii kugongana na pale ambapo hilo linaonekana bila kufanyiwa kazi ni wazi kuwa lipo tabaka litaibuka na kuonesha hisia zake,” amesema.

Amsema kwa fikra zake anaamini jamii nzima ikishirikishwa kurejesha nchi kwenye hali yake inawezekana, huku akitoa tahadhari kuwa hilo halihitaji kundi fulani kwani nchi imechanikia mikononi kwa watu wote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here