Home KITAIFA Hakuna mtoto atakayezuiwa kusoma kwa kukosa sare za shule

Hakuna mtoto atakayezuiwa kusoma kwa kukosa sare za shule

Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha hakuna mtoto anayezuiwa kuanza au kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa  sare za shule (unifomu) wakati shule zote nchini zikitarajiwa kufunguliwa rasmi Januari 13, 2025.

Amesema kuwa agizo hilo linapaswa kusimamiwa kikamilifu katika maeneo yote ya nchi ili kuhakikisha kila mtoto anapokelewa shuleni bila masharti yanayokiuka miongozo na sera za elimu.

Amesisitiza kuwa mara mtoto anapopokelewa shuleni, masuala mengine ikiwemo unifomu yataendelea kushughulikiwa akiwa tayari anaendelea na masomo, hatua itakayosaidia kuondoa vikwazo vinavyowafanya baadhi ya watoto kukosa haki yao ya msingi ya elimu.

Aidha, Profesa Shemdoe amekemea tabia ya baadhi ya shule za serikali kuweka michango mingi kwa wazazi, ikiwemo kuwalazimisha kununua unifomu shuleni, akieleza kuwa hatua hiyo ni kinyume na taratibu na miongozo ya Serikali.

Ameelekeza walimu wakuu, walimu na viongozi wa shule kusoma, kuelewa na kuzingatia miongozo ya elimu iliyopo, pamoja na kutoa elimu sahihi kwa wazazi na walezi ili kuondoa sintofahamu zisizo za lazima.

“Lengo la Serikali ni kuona watoto wote wanakwenda shule bila vikwazo vyovyote, na kuhakikisha hakuna mtoto anayenyimwa haki yake ya elimu kwa sababu ya changamoto za kiuchumi au maamuzi yasiyo sahihi,” amesisitiza Profesa Shemdoe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here