Na Mwandishi Wetu,Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar ameishauri Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kuongeza ubunifu katika kushirikiana na Serikali pamoja na Sekta binafsi ili kuchangia katika maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ametoa ushauri huo jijini Dodoma alipokutana na kuzungumza na uongozi wa benki hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na fursa za ushirikiano kati ya Serikali na benki hiyo, katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square.
Balozi Omar amesema kuwa benki hiyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ikitumika vizuri inaweza kuufanya Ukanda huo kuwa mfano wa ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.
“Kasi ya maendeleo yanayotokana na benki hiyo ikionekana vizuri tutakuwa wa mfano na kuiwezesha jumuiya nyengine kama Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuja kujifunza kwetu,” amebainisha Balozi Omar.
Aidha amesema kuwa ni muhimu pia kwa benki hiyo kuchangia katika kupunguza umaskini ikiwa ni pamoja na kujenga ujuzi na ustadi unaoendana na mahitaji ya kiuchumi, na mipango ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu.
Ameishauri pia benki hiyo kujitangaza ili kuwawezesha wananchi hususan Sekta Binafsi waweze kutambua fursa mbalimbali zinazo patikana katika benki hiyo.
“Jukumu lenu ni kuhakikisha wateja wanaifahamu zaidi benki pamoja na fursa zake,”amesisitiza.
Aidha, ameipongeza benki hiyo kwa mipango na michango mbalimbali ambayo imekuwa ikichangia katika maendeleo ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Tanzania.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Dk. Charles Mwamwaja, alisema benki hiyo ilianzishwa mwaka 1967 kwa lengo la kuchangia katika kukuza maendeleo ya kiuchumi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema benki hiyo imeandaa mkakati madhubuti wa kuwawezesha wadau kufahamu fursa mbalimbali zinazopatikana katika benki hiyo kwa kuwa benki hiyo haifanyi kazi na Serikali pekee bali hata sekta ninafsi katika kuleta maendeleo.
Aidha, ameahidi kuyafanyia kazi kikamilifu maaelekezo na ushauri uliotokewa na Mhe. Waziri ili kuwezesha nchi kukamilisha mipango yake na kufikia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB),Benard Mono, alisema kuwa benki hiyo ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika miradi ya maendeleo ili kuzalisha ajira na kuongeza thamani katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
Mono ameongeza kuwa wapo tayari kutoa mikopo katika sekta za umma pamoja na sekta binafsi kwa kuzingatia vigezo vya mkopeshwaji kwa lengo la kujenga Uchumi imara kwa nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, kama lilivyo lengo la benki hiyo kuanzishwa la kuchochea maendeleo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Amina Khamis Shaaban, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Rished Bade, Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Stephen Wambura na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha.



